Kenya. Unakumbuka hii? Kuna simulizi maarufu iliyochukua miongo kadhaa katika nchi ya Kenya.

Ni kisa kinachomhusu mwanamuziki wa DR Congo, Kanda Bongoman kudaiwa kuingilia uhusiano wa mapenzi kati ya Rais wa zamani, hayati Daniel Toroitich Moi na mtangazaji Catherine Kasavuli (naye ni marehemu).

Kisa hicho ndicho kinachodaiwa kusababisha Kanda Bongoman kufukuzwa ghafla mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Ilikuwa simulizi iliyonong’onezwa vijiweni na kwenye baa, ikirudiwa kwenye vipindi vya redio na kuthibitishwa kama ni tukio la kweli. Lakini siku zote, uongo huwa unapanda lifti na ukweli huwa unakuja taratibu kwa kupanda ngazi.

Hivyo, chini ya uvumi huo kuna ukweli tofauti kabisa na tukio lenyewe jinsi lilivyochukuliwa na jamii. Ukweli unaofichua kwamba tukio hili lilitokana na ubabe, kiburi na siasa.

Ili kuelewa, mtu lazima arudi mwanzoni mwa mwaka 1990, wakati muziki wa Soukous ulipotawala Bara la Afrika.

Mdundo wa Congo ulivuma na kubebwa na magitaa yaliyong’ara na dansi la KwasaKwasa lililokuwa na hisia kali, ulikuwa muziki unaovutia mioyo kutoka Kinshasa hadi Nairobi na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Wakenya walimpenda sana Kanda Bongo Man, mwimbaji wa DR Congo mwenye haiba ambaye tabasamu lake la kuambukiza na msisimko usiozuilika ulimfanya kuwa mmoja kati ya wanamuziki wa kigeni maarufu zaidi wa wakati huo.

Wimbo wake maarufu Inde Monnie ulitawala mawimbi ya hewa ya Kenya, ukivuma kutoka katika matatu (daladala) na klabu za usiku pia. Ulikuwa muziki ulioamua enzi na kuwafanya watu wacheze pamoja.

Mwaka 1991, mtangazaji mkongwe Fred Obachi Machoka alimwalika Bongoman kwenda kutumbuiza Kenya chini ya Sauti ya Kenya (sasa KBC). Mwitikio ulikuwa mkubwa sana.

Maonyesho ya Kanda Bongoman katika Viwanja vya Carnivore, Bomas, KICC na Uwanja wa Nyayo yalivutia umati usio wa kawaida.

Ilipotimu Aprili 7, 1991, Uwanja wa Nyayo ulifurika mashabiki zaidi ya 40,000 wenye furaha, Makamu wa Rais Profesa George Saitoti alihudhuria akiwa sehemu ya VIP, gwiji wa Kikuyu Joseph Kamaru alikuwa jukwaani, na Fred Machoka aliongoza sherehe.

Ulikuwa usiku wa dhahabu kwa burudani ya Kenya, mkutano wa midundo, vipaji, na furaha.

Lakini siku chache baadaye, furaha hiyo iligeuka na kuwa mkanganyiko na ukimya. Muda mfupi baada ya onyesho lake la Nyayo, Kanda alipangiwa kutumbuiza katika Hoteli ya New Stanley.

SAA 24 KUONDOKA

Bendi ilipokuwa ikijiandaa, msafara wa maofisa waliovalia nguo za kiraia ulifika kutoka Ikulu na kumtaka mwanamuziki huyo aondoke Kenya ndani ya saa 24. Hakuna maelezo yaliyotolewa.

Asubuhi iliyofuata, Kanda Bongoman alikuwa ameondoka, akisindikizwa hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta na kupandishwa ndege inayofuata.

Ukimya rasmi ulitawala na kuacha nafasi kwa uvumi kuibuka na kuchukua nafasi. Minong’ono ilidai kwamba Bongoman alikuwa amefukuzwa kwa kujihusisha kimapenzi na Kasavuli, mtangazaji pendwa wa habari wa KTN Kenya na mwanamke anayeaminika kuwa alikuwa karibu na Rais Moi. Simulizi hiyo ilikuwa ya kusisimua sana na imedumu kwa miongo kadhaa sasa.

Hata hivyo, kadiri miaka inavyopita wale waliokuwapo walianza kuzungumza na kumbukumbu zao zilisimulia kisa tofauti kabisa.

UKWELI DHAHIRI

Katika mahojiano yaliyofanywa hivi karibuni nchini Kenya kati ya mtangazaji wa redio, Patrick Igunza na Fred Obachi Machoka, hatimaye ukweli ulibainika.

Machoka alipuuza kuhusu uvumi huo moja kwa moja, akakumbuka usiku wa tukio la kufukuzwa lilivyoanza na kuzua machafuko.

“Tulikuwa na kila kitu tayari, jukwaa, sauti, wanamuziki na wanenguaji walishapanda,” alisema.

“Kisha ghafla, maafisa walitokea na kusema, hakuna onyesho na kudai ni maagizo kutoka juu. Walitaka nitangaze, lakini nilikataa. Umati ungekuwa na hasira sana.”

Hatimaye, meneja mkuu wa hoteli hiyo, Alphayo Onyango, alitoa tangazo hilo. Wananchi walilipuka kwa hasira, wakavunja viti, meza na vikombe wakipinga kutokuwapo kwa onyesho hilo.

APANDISHWA NDEGE

Machoka alisema baada ya kushuhudia tukio hilo, alikimbilia katika chumba maalumu ambako alimkuta Kanda Bongoman akiwa ameshajiandaa kwa kuvaa nguo zake tayari kupanda jukwani kutumbuiza.

“Nilimwambia Bongoman kwamba polisi walikuwa wamefuta onyesho lake,” anakumbuka Machoka.

“Ndani ya dakika chache, maofisa walikuwa mlangoni. Walimwambia lazima aondoke kwenye ardhi ya Kenya mara moja.”

Kanda alipowaambia kwamba ndege yake ya Air France ilikuwa tayari imeondoka, maofisa walisisitiza achukue inayofuata.

Machoka anasema yeye alimpeleka Bongoman hadi kwenye uwanja wa ndege na akabaki hadi pale ndege ilipopaa.

Machoka anakumbuka alimuuliza mmoja kati ya maofisa kwanini Bongoman amefukuzwa, mtu huyo alirudia uvumi huo kuhusu Kasavuli kwa njia isiyo ya kawaida.

Lakini Machoka, ambaye alikuwa na Bongoman karibu kila siku, hakuuamini uvumi huo.

“Niliwahi kumuuliza Bongoman kama hata anamfahamu Kisavuli. Alionekana kuchanganyikiwa na akasema hajawahi kukutana naye. Nilimwamini,” anasimulia Machoka.

Akiwa amedhamiria kujua sababu halisi, Machoka alifanya uchunguzi na kugundua maelezo tofauti kabisa na sababu iliyotolewa ili kumfukuza Bongoman Kenya.

KISA HARUSI YA KIGOGO

Sababu mojawapo ilitokana na kiburi na misuli ya kisiasa. Wakati akiwa katika Hoteli ya Intercontinental, Bongoman alifuatwa na wasaidizi wa Hezekiah Oyugi, mmoja kati ya makatibu wakuu waliokuwa na nguvu katika Serikali ya Rais Moi.

Wasaidizi hao walimtaka mwanamuziki huyo akatumbuize kwenye harusi ya binti wa Oyugi huko Rongo.

Rongo ni mji uliopo Kusini Magharibi mwa Kenya katika Kaunti ya Migori, takriban kilomita 30 Kaskazini Mashariki mwa Migori.

Kanda alikataa kwa heshima zote, akisema hataweza kutumbuiza kwenye sherehe za faragha na alimpendekeza msanii mwenzake wa DR Congo, Elisabeth Muidikay maarufu kama Tshala Muana, ambaye pia alikuwa Nairobi wakati huo akatumbuize katika sherehe hiyo.

Hata hivyo, kukataa huko hakukumpendeza Oyugi. Kwa kutumia ushawishi wake na ukaribu wake na mamlaka, inadaiwa alilitaja jina la Rais Moi na kuamuru mwanamuziki huyo aondolewe Kenya.

Katika mahojiano ya mwaka 2024 na Radio Maisha, Kanda alithibitisha simulizi hii, hatimaye akasafisha jina lake baada ya zaidi ya miongo mitatu ya uvumi.

“Oyugi aliniomba nikatumbuize kwenye harusi ya binti yake, Rose,” alisema Bongoman.

“Lakini visa yangu ilikuwa inakaribia kuisha muda wake. Nilimwambia nilihitaji kuiboresha, aliniambia nisijali, yeye ni mtu mkubwa katika ofisi ya Rais.’

Lakini Oyugi alipompigia simu afisa wa uhamiaji, Bw. Kuinga aliposikia kuhusu nguvu aliyoitumia, alikataa kuiboresha visa yangu.

Kuinga alisema, “nitamwonyesha kama mimi pia ni mtu mkubwa. Hapo ndipo waliponiondoa kabla sijafanya onyesho.”

Kuhusu uvumi unaomhusisha na Kasavuli, Bongoman aliukataa kabisa, akifafanua alikutana na mwanamke huyo kwa mara ya kwanza mwaka 2005, kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, aliporudi Kenya baada ya kualikwa rasmi na Waziri wa Utalii na Habari wa wakati huo Raphael Tuju.

Kufikia wakati huo, majeraha yalikuwa yamepona, hadithi za uongo zilikuwa zimefifia na mdundo ulikuwa umerudi tena nyumbani.

Kwa muda mrefu sasa, umma uliamini simulizi iliyojengwa juu ya uvumi ambayo iliongeza mateso kwa mwanamuziki maarufu kwa kashfa ya bei rahisi. Lakini kama ukweli unavyoonyesha sasa, kufukuzwa kwa Kanda Bongoman pale Kenya hakukuwa kwa sababu ya masuala ya kimapenzi, bali la ushindani na ubinafsi pamoja na madaraka kwa vigogo wa serikali ya Kenya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *