Serikali ya Libya imetangaza kuwa itaongeza kasi ya kuwarejesha makwao wahamiaji wasio halali wa Kiafrika wa nchi za chini ya Jangwa la Sahara, lakini imesema, kwa upande wa wakimbizi wa Sudan watachukuliwa kama Walibya na kuruhusiwa kupata huduma za skuli na hospitali.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Libya Imad Trabelsi amebainisha hayo katika mkutano na waandishi wa habari aliofanya mjini Tripoli akiwa pamoja na mabalozi kadhaa wa kigeni na akatoa ombi kwa Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika, na nchi za Kiarabu kutoa misaada zaidi ili kuweza kuwahudumia wahajiri na wakimbizi walioomba hifadhi nchini humo.

Trabelsi ameongeza kuwa, Libya imepokea msaada ‘mdogo sana’ ikilinganishwa na ‘ahadi kubwa’ ilizotoa za kushughulikia tatizo hilo.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Libya ameeleza kwamba, karibu wahamiaji milioni tatu wamekuwa wakiishi nchini humo katika kipindi cha miaka 15 iliyopita na kubainisha kwamba, mpango wa taifa wa kuwarejesha katika nchi zao wahamiaji wasio halali umekuwa ukiendelea tangu mwezi Oktoba, ukiwa na malengo mwezi huu ya ‘kurejesha maelfu ya wahamiaji’, ikiwa ni pamoja na wengi kuelekezwa Chad, Somalia na Mali.

Trabelsi amesema kuhusu mamia ya maelfu ya wakimbizi wa Sudan walioingia Libya wakikimbia vita nchini mwao kwamba ‘maelekezo ya serikali ni kuwa watatendewa kama Walibya na waruhusiwe kupata huduma za afya na masomo’.

Ameongeza kuwa, hadi sasa wakimbizi 700,000 kutoka Sudan wamewasili huko Libya tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipoanza nchini humo Aprili 2023…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *