
Badala ya utulivu waliouhitaji hii Alhamisi asubuhi, wakaazi wa maeneo ya Kaziba, Kamanyola, Katogota na Lubarika waliamka tena wakisikia milio mizito ya mabomu na bunduki kutoka kwenye milima ya Bufuliru wilayani Uvira na katika milima ya Walungu.
Kuongezeka kwa mapigano kunazidisha kuzorota kwa hali ya kibinadamu, ambayo tayari ilikuwa ngumu tangu kuanza kwa mashambulizi ya AFC/M23 katika Kivu Kusini. Wakazi wanasema vita vimewakumba wakiwa hawana hata akiba ya chakula majumbani.
Katika taarifa yake ya kutetea amani, Chama cha Wanahabari Wanawake Waliojitolea kwa Amani (AFJEP/Kamituga) kimeonya kuhusu kuzorota kwa hali ya kibinadamu kwa wakimbizi wa ndani katika eneo la Mwenga, ambalo pia limeathiriwa na mapigano. Immaculée Chakupewa, mratibu wa shirika hilo, anatoa wito wa kuchukuliwa hatua za dharura.
Jean-Chrisostome Kijana, mwanachama wa jukwaa la wananchi Pamoja kwa Amani, amesema ameshangazwa na kuongezeka kwa vurugu wakati viongozi wa Rwanda na Kongo wakitarajiwa kutia saini mkataba wa amani.
Milio ya risasi imesikika pia Alhamisi asubuhi katika kijiji cha Mudaka, takriban kilomita 15 kaskazini mwa Bukavu ambako wakazi wamesema wanamgambo wa Wazalendo walijaribu kuvuruga usalama, na kwamba vikosi vya AFC/M23 vilielekea eneo hilo katika juhudi za kurejesha utulivu.