DW Access: Mwitikio wa wakati muafaka dhidi ya ukandamizaji wa uhuru wa habari duniani
Kuanzia wazo la awali hadi toleo rasmi ndani ya miezi minane pekee, uundwaji wa DW Access ulianza katika shindano la ubunifu la ndani la DW lijulikanalo kama “Hacking for Freedom”.
Tayari kufikia Machi 2025, umuhimu wa kuchukua hatua ulikuwa dhahiri: Upatikanaji wa DW katika nchi kama Urusi, China, Iran na Uturuki ulikuwa umeanza kutegemea sana matumizi ya VPN au majukwaa yaliyozuiliwa. Kufikia katikati ya mwaka 2025, ukandamizaji wa mtandaoni na kuzimwa kwa intaneti viliongezeka, hususan nchini Iran wakati wa “Vita vya Siku Kumi na Mbili” na Israel, pamoja na nchini Afghanistan na Burkina Faso. Hali hii inayozidi kuwa ngumu iliibua swali: DW ingewezaje kutoa njia ya kuaminika ya kufikia habari huru katika maeneo ambako hali ya mtandao na udhibiti hubadilika bila kutabirika?
Ndipo, katika kusanyiko la Machi, wataalamu wa DW, Okay Suna na Ingo Felscher, wakaanza kuunda toleo la mwanzo la programu hiyo. Baadaye, Okay alitumia muda wa miezi minane akiendeleza zaidi wazo hilo huku mmiliki wa bidhaa hiyo Dominik Krull, timu ya uendelezaji wa bidhaa za kidigitali na timu yake ya wabunifu wa programu – wakichukua uongozi wa mradi huo.
Kadiri mradi ulivyopiga hatua, kitengo cha Ubunifu cha UX/UI, kwa ushirikiano mkubwa kutoka kwa Annette Diegel-Ruppert (UX) na Ewa Kwade (UI), kilibuni muonekano na matumizi ya programu, kikihakikisha pia kuwa inalingana na chapa ya DW. Kitengo cha Masoko cha DW kilitengeneza jina la programu, uimara wa chapa yake na mkakati wa kuizindua.
Oliver Linow na Esther Kleine kutoka timu ya Internet Freedom walifanya kazi kama kiungo kati ya wahandisi wa programu na mashirika ya teknolojia yanayojikita katika uhuru wa mtandao. “Hatimaye tumepata suluhisho linalosaidia si tu DW, bali pia kuwalinda watumiaji wetu na kufanya kazi hata katika mazingira magumu zaidi,” anasema Esther Kleine, Meneja wa Mradi wa Internet Freedom. “Tungependa kuwashukuru wote waliohusika kwa kujitolea kwao kwa kiwango cha hali ya juu katika mradi huu,” anaongeza Oliver Linow.
DW Access yazaliwa
Ushirikiano huu kati ya idara mbalimbali uliwezesha kuzaliwa kwa DW Access – programu tumishi nyepesi, isiyodhibitika kirahisi, na iliyoundwa mahsusi kwa masoko yenye mazingira tete ya kidijitali. Timu hii shirikishi sasa inaanza hatua inayofuata ya maendeleo: kutengeneza stealth mode, yaani hali fiche itakayofanya programu hiyo isitambulike hata wakati wa ukaguzi wa vifaa.
Haipatikani kimakusudi kwenye maduka ya kawaida ya app
DW Access iliundwa kama jibu kwa ongezeko la udhibiti wa intaneti duniani unaofanywa na serikali mbalimbali, lakini pia ili kutoa jukwaa huru kwa watumiaji—lisilotegemea makampuni makubwa ya teknolojia na ushawishi wao. DW Access inafanya kazi nje ya mifumo ya kawaida ya upakuaji wa app, ikiruhusu watumiaji kuisambaza kwa wengine kupitia kiungo cha kupakua, au hata kwa kutuma faili moja kwa moja kupitia huduma za ujumbe au Bluetooth.
“Kwenye Android, app yetu mpya ya DW Access ina VPN iliyojengewa ndani iitwayo Outline, utambuzi usioeleza utambulisho wa kifaa, na haipeleki data yoyote binafsi—hatua muhimu kuhakikisha usalama wa watumiaji,” anaeleza Ingo Mannteufel, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA na Usalama wa Mtandao. “Android inatumika sana katika nchi lengwa za programu hii—hasa katika maeneo yenye udhibiti—na njia zake za usambazaji zinaendana kikamilifu na mkakati wetu wa kuendesha app nje ya maduka rasmi ya programu.”
Kwa sababu ya masharti makali ya udhibiti wa maudhui, DW Access kwa sasa haipatikani kwenye iOS.
Inafanya kazi hata bila mtandao kabisa
Zaidi ya hapo, DW Access ina uwezo wa kufanya kazi mtandaoni na nje ya mtandao. Miongoni mwa vipengele hivyo ni huduma ya kushirikisha makala, inayowawezesha watumiaji kutuma makala kama viungo au kama faili za PDF kupitia Bluetooth. Kupitia kipengele cha kuokoa matumizi ya data, programu inaendelea kufanya kazi hata pale mtandao wa simu unapopunguzwa kasi. Watumiaji wanaweza kuchagua kupunguza matumizi ya data—kwa mfano kwa kupakia maandishi pekee—ili kurahisisha ufikaji wa maudhui. Zaidi ya yote, iwapo mtandao utakosekana kabisa, programu bado inaweza kutumika kwa sababu ya mfumo wa kuhifadhi maudhui mapema (pre-caching).
Jinsi ya kuipata
DW imeanzisha tovuti mpya, access-unlocked.org, kwa lengo la kuwasaidia watumiaji wakati wa matukio ya udhibiti wa intaneti. Kupitia tovuti hiyo, watumiaji wanaweza kupata viungo vya moja kwa moja vya kupakua DW Access. Aidha, DW inashirikiana na duka la programu la Paskoocheh kwa usambazaji wa programu hiyo nchini Iran.
DW Access inakamilisha programu ya sasa ya “DW – Breaking World News”, ambayo bado inapatikana kupitia maduka rasmi ya programu. Kwa maoni na mrejesho, watumiaji wanaweza kuwasiliana kupitia: internet-freedom@dw.com
Vidokezo muhimu
• Tumia programu kwenye simu binafsi. Simu zinazosimamiwa na taasisi au waajiri (kwa mfano, simu za kazini) mara nyingi huzuia upakuaji au usakinishaji wa programu kutoka nje ya maduka rasmi (sideloading).
• Kusambaza programu, tumia njia kama ujumbe kupitia programu za mawasiliano (mfano Signal au WhatsApp), Bluetooth, au kwa kutuma kiungo cha ukurasa huu: www.access-unlocked.org
.• Epuka kuituma kwa barua pepe, kwa kuwa viambatisho vya aina ya faili kama hii (.apk) mara nyingi hutua kwenye folda ya barua taka au vinaweza kukataliwa na mfumo kabla hata havijatumwa.
• Hata hivyo, barua pepe, programu za ujumbe, au hata taarifa kwa njia ya maneno vinafanya kazi vizuri kwa kushiriki kiungo cha tovuti: www.access-unlocked.org