Matamshi ya dharau yaliyotolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump, kuhusu watu na nchi ya Somalia yamesababisha wimbi la hasira na majibu makali.

Shirika la Habari la Reuters limeripoti kuwa, Wasomali wamejibu kwa hasira matamshi ya kukera ya Trump, wakiyataja kuwa ni ya kibaguzi.

Akizungumza katika kikao cha baraza lake la mawaziri, Donald Trump, alidai kuwa Wasomali wamepora mabilioni ya dola ya jimbo la  Minnesota bila kuchangia chochote, na kuwaita “takataka”.  Aliongeza kuwa “Nchi yao haina maana, inanuka, na hatuwataki nchini Marekani.”

Matamshi hayo ya Rais wa Marekani yanafuatia mashambulizi yake ya maneno dhidi ya wahamiaji wa Kisomali. 

Ripoti ya Reuters inasema: Abdulsalam Omar, ambaye ni miongoni mwa wazee wa Somalia, amesema “ameshtushwa” na kauli hizo na kusisitiza kwamba “dunia lazima ijibu matamshi hayo.” 

Bole Ismail, mfanyakazi mwenye umri wa miaka 45 mkazi wa Mogadishu, pia amesema: “Maneno kama hayo hayapo katika utamaduni wetu… Watu wa Marekani wanapaswa kwanza kumghadhabikia Trump na kumpeleka kwenye vituo vya uchunguzi wa magonjwa ya akili.”

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Somalia, Hamza Abdi Barre, pia ameashiria matamshi ya Rais wa Marekani dhidi ya Somalia na Wasomali na kusema: “Maneno mengine hayafai kujibu na ni bora yapuuzwe.”

Gavana wa Minnesota huko Marekani, Tim Walz, amejibu matamshi ya chuuki ya Trump kwa kuwasifu Wasomali wa eneo hilo huku akimtuhumu Rais huyo wa Marekani kuwa ‘anadhalilisha kundi zima la watu waliokimbia vita na kuunda jamii yenye nguvu inayoboresha Minnesota na Marekani.’

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *