Uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi karibuni umebaini kuwa, karibu nusu ya raia wa nchi wananchama wa Umoja wa Ulaya, EU wanamwona Rais wa Marekani Donald Trump kama “adui wa Ulaya,” huku wengi miongoni mwao wakihisi hatari ya kuzuka vita vya wazi baina ya nchi zao na Russia katika miaka ijayo kuwa ni ya “juu”.

Kwa mujibu wa taasisi ya Eurobazooka yenye makao yake makuu nchini Ufaransa, matokeo ya uchunguzi huo wa maoni uliofanywa na taasisi ya uchunguzi wa maoni ya Cluster 17 na kuchapishwa jana Alkhamisi na jarida la Le Grand Continent yanaonyeshwa kuwa idadi ya Wazungu wanaomwona Trump kama “adui” wa Ulaya ni asilimia 48, likiwa ni ongezeko la pointi nne kulinganisha na utafiti uliopita uliofanywa mwezi Septemba.

Utafiti huo pia umegundua kwamba asilimia 51 ya raia hao wa nchi wanachama wa EU wanahisi hatari ya kuzuka vita vya moja kwa moja kati ya nchi zao na Russia katika miaka ijayo kuwa iko “juu,” huku asilimia 18 wakisema hatari hiyo ni ya “juu sana.”

Halikadhalika, zaidi ya theluthi mbili ya waliohojiwa na kutoa maoni yao, yaani asilimia 69, wanaamini kuwa nchi zao hazingeweza kujihami endapo zingeandamwa na shambulio la kijeshi la Russia, huku kiwango hicho kikiongezeka na kuwa zaidi ya 80% katika nchi za Ureno, Italia na Ubelgiji.

Utafiti huo umebaini pia kwamba asilimia 55 ya waliohojiwa wanafadhilisha nchi zao kujiweka umbali sawa na Marekani na China, badala ya kujiunga na kuwa karibu karibu na moja tu kati ya madola hayo.

Uchunguzi huo wa maoni umefanywa katika nchi tisa za Ulaya, ambazo ni Ufaransa, Italia, Uhispania, Ujerumani, Poland, Ureno, Croatia, Romania, na Ugiriki…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *