
Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kimeanza mazoezi makubwa katika Ghuba ya Uajemi, kikionyesha uwezo wa hali ya juu wa kujilinda na kushambulia ulioimarishwa kwa akili mnemba.
Jeshi la Wanamaji la IRGC lilianza mazoezi hayo jana Alhamisi, likisisitiza utayarifu ulioimarishwa wa kijasusi na kuonyesha ari isiyoyumba na uimara wa wanamaji wake wa kukabiliana na tishio lolote.
Wakati wa mazoezi hayo, vitengo vya majini vya IRGC vimewasilisha ujumbe madhubuti kwa kutoa maonyo kwa meli za kivita za Marekani zilizokuwepo katika eneo hilo.
Mifumo ya kisasa ya ulinzi wa anga ikiwa ni pamoja na Nawab, Majid na Misagh pia imetumika katika hali ya vita vya kielektroniki. Kwa kutumia akili mnemba, mifumo hiyo iliweza kutambua malengo ya angani na ya majini kwa muda mfupi na kuyapiga kwa usahihi wa hali ya juu.
Mazoezi hayo ya kijeshi, yaliyopewa jina la Shahid Mohammad Nazeri, yanafanyika katika Ghuba ya Uajemi, eneo la baharini la Nazeat – Abu Musa, Tonb Kubwa, Tonb Ndogo, na visiwa vya Siri, Mlango-Bahari wa Hormuz, pamoja na Bahari ya Oman.
Nazeri alikuwa kamanda wa kikosi maalumu cha makomandoo cha Wanamaji wa IRGC. Anatambulika sana nchini Iran kwa kuhusika kwake moja kwa moja katika kutekwa mabaharia 10 wa Marekani – wanaume tisa na mwanamke mmoja – walioingia katika maji ya eneo la Iran mnamo Januari 12, 2016.
Maneva hayo yanatoa ujumbe wa pande mbili: amani na urafiki kwa nchi jirani, na onyo la wazi kwa maadui kwamba makosa yoyote yatakabiliwa na jibu la haraka.
Vikosi vya majini vya Iran na Marekani vimekuwa na historia ndefu ya mapigano katika Ghuba ya Uajemi, Bahari ya Oman, na Mlango-Bahari wa Hormuz tangu miaka ya 1980.
Jeshi la Wanamaji la Iran mara nyingi hufanya mazoezi makubwa katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman, kuonyesha uwezo wake na nguvu ya kukabilia na mataifa ya kigeni.