
Tangu kuanza kwa vita katika nchi jirani ya Sudan mwezi Aprili 2023, Chad inakabiliwa na wimbi kubwa la wakimbizi. Ili kufanya kazi na kufikisha misaada kwa walengwa, mashirika ya Umoja wa Mataifa karibu kila mara hulazimika kutumia wasindikizaji wenye silaha ili kuhakikisha usalama wao, tofauti na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali ambayo husafiri bila wasindikizaji.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Lakini katika muktadha wa kupunguzwa kwa ufadhili wa Magharibi, gharama ya wasindikizaji hawa inadhoofisha shughuli za kibinadamu. Wafanyakazi walio katika kambi mbalimbali za wakimbizi wanatoa wito kwa mamalaka ya Chad kubadilika.
“Matumizi ya kimfumo ya wasindikizaji wa kulipwa mashariki (…) yanazidisha changamoto za kifedha,” inaonya OCHA, ofisi ya uratibu wa kibinadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Chad, katika taarifa ya tarehe 27 Novemba.
Kulingana na makubaliano yaliyopo ya kusafiri mashariki mwa Chad, Umoja wa Mataifa unapaswa karibu kila mara kutumia kitengo cha DPHR, Kikosi cha Ulinzi wa wakimbizi na Wafanyakazi wa Kibinadamu, kitengo maalum cha polisi.
Kiutendaji, kila safari inahitaji malipo ya kukodisha gari, mafuta, na posho ya kila siku kwa kila polisi anayesindikiza msafara wa magari ya mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa. Kwa Umoja wa Mataifa, wasindikizaji hawa wanawakilisha bajeti ya zaidi ya dola 900,000 kwa mwaka 2024 pekee. Hii inatosha kutoa msaada kwa zaidi ya Wachad 3,000 katika eneo hilo au zaidi ya wakimbizi 1,700 wa Sudan, kulingana na hati hiyo.
Wausika hupata pesa nyingi
Katika eneo hilo, baadhi ya shughuli za usaidizi kwa wakimbizi wakati mwingine hufutwa kutokana na ukosefu wa wasindikizaji, mkuu wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa ametuambia. “Kila dola inayotumika kwa wasindikizaji hupunguza uwezo wa kuokoa maisha ya watu,” inasema OCHA, ambayo inarudia kwamba, kimsingi, “wasindikizaji wenye silaha wanapaswa kubaki kama hatua ya mwisho, kutokana na vitisho vilivyoko.”
Miongoni mwa wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu, kuna makubaliano kwamba wasindikizaji bado ni muhimu katika baadhi ya maeneo ambapo wizi ni wa mara kwa mara, lakini kwamba mamlaka zinaweza kuwa rahisi zaidi kuhusu njia fupi na salama. Majadiliano kuhusu mada hii yamekuwa yakiendelea na serikali kwa zaidi ya mwaka mmoja, lakini yanazuiwa na “kutokuwa na utashi kutoka mamlaka ya ndani, kwa sababu kuna pesa nyingi wanazopata,” kulingana na mfanyakazi wa shirika moja la kutoa misaada ya kibinadamu akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina.
OCHA inatetea suluhisho mbadala zinazohusisha serikali ya Chad na washirika wake, bila kutaja suluhisho hizo zinaweza kuwa zipi. OCHA wala serikali hawakupatikana mara moja kutoa maoni yao.