Washington DC, Marekani. Droo ya upangaji makundi ya Fainali za Kombe la Dunia 2026 iliyofanyika juzi Washington DC, Marekani imetengeneza mechi za mvuto na ushindani za mashindano hayo ambayo yatafanyika katika nchi za Canada, Mexico na Marekani.
Ni droo ambayo inaleta matumaini kwa timu nyingi zilizo juu kwenye chati ya ubora wa soka duniani kusonga mbele na kutinga hatua inayofuata ya 32 bora.
Matumaini Afrika
Namna makundi hayo yalivyopangwa, inaleta matumaini kwa timu nyingi zinazowakilisha Bara la Afrika kusonga mbele kwani hazionekani kama zitashindwa kuvuna pointi za kuzifanya zimalize katika nafasi mbili za juu kwenye makundi au kupata nafasi nane za ziada ambazo zitakuwa kwa timu zenye matokeo mazuri zitakazomaliza katika nafasi ya tatu.
Afrika Kusini imepangwa kundi A ambalo litakuwa na mwenyeji mwenza Mexico, Korea Kusini na timu nyingine itakayofuzu kupitia mchujo.
Morocco imeangukia kundi C ambalo lina Brazil, Scotland na Haiti huku Ivory Coast ikiwa kundi E lenye Ujerumani, Ecuador na Curacao.
Tunisia itakuwa na kibarua katika kundi F ambalo litakuwa na Uholanzi, Japan na timu nyingine itakayopatikana kupitia mechi za mchujo na Misri imepangwa kundi G pamoja na Ubelgiji, Iran na New Zealand.
Cape Verde itakuwa pamoja na Hispania, Saudi Arabia na Uruguay katika kundi H na wawakilishi wengine wa Afrika, Senegal wao wamepangwa kundi I na Ufaransa, Norway na timu moja ambayo itapatikana kupitia hatua ya mchujo.
Algeria ipo kundi J na mabingwa watetezi Argentina, Austria na Jordan wakati huo Ghana ikipangwa kundi L ambalo pia lina England, Panama na Croatia.
Mechi za moto
Kabla hata haijachezwa, mechi ya kundi A baina ya Mexico na Afrika Kusini imeonekana kuwa gumzo kwa wapenzi wengi wa soka duniani.
Timu hizo zitaweka rekodi ya kukutana mara mbili katika mechi ya ufunguzi wa Fainali za Kombe la Dunia kwani mara ya kwanza zilifabya hivyo mwaka 2010 wakati mashindano hayo yalipofanyika Afrika Kusini ambapo zilitoka sare.
Kutakuwa na marudio ya nusu fainali ya Kombe la Dunia 2018 baina ya Croatia na England kwa vile timu hizo zimepangwa kundi moja.
Kitendo cha Senegal kupangwa kundi I pamoja na Ufaransa hapana shaka kunafanya mechi baina yao kukumbushia mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia 2002 ambao Senegal iliichapa Ufaransa kwa bao 1-0.
Makocha watia neno
Kocha wa Morocco, Walid Regragui amesema kuwa anafurahia kuona timu yake ikipangwa kundi moja na Brazil huku akikutana nayo katika mechi ya kwanza.
“Kucheza na Brazil ni ndoto ya kila mmoja. Brazil ni nchi ya mpira wa miguu na kwa Wamorocco, ni mfano. Tuna heshima kubwa kwa Brazil lakini tuwe wa kweli, itakuwa ni mechi kubwa. Timu bora ishinde,” alisema Regragui.
Mauricio Pochettino anayeinoa Marekani, amewataka wachezaji wake kuzipa heshima timu zote walizopangwa nazo kwenye kundi D.
“Ujumbe wangu kwa wachezaji, Paraguay, Australia na timu nyingine (mshindi wa mchujo) zitakuwa ngumu. Tunahitaji kujiandaa kama vile kila mchezo ni fainali ya Kombe la Dunia. Kufikiri tunapaswa kushinda kabla ya kucheza michezo ni mawazo yasiyofaa,” alisema Pochettino.
Kocha Mkuu wa Misri, Hossam Hassan alisema, “Misri ina malengo yenye uhalali na nafasi ya kweli ya kufika mbali iwezekanavyo. Tutazingatia kazi yetu, na tuna muda baada ya Kombe la Mataifa ya Afrika, ambayo itakuwa fursa nzuri ya maandalizi ya Kombe la Dunia.
“Yeyote anayetaka kufika mbali na kuleta furaha kwa mashabiki lazima afanye kazi kwa bidii na kujituma.”