Dar es Salaam. Mechi mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara zinachezwa leo katika viwanja na miji tofauti lakini habari kubwa zaidi ni ile inayokutanisha Simba na Azam FC katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 11:00 jioni.

Mvuto wa mchezo baina ya Simba na Azam FC unatokana na mwenendo wa timu hizo katika ligi msimu huu unaolazimisha kila moja kuhakikisha inapata ushindi leo.

Wenyeji Simba ambao hawajapoteza wala kutoka sare katika mchezo wowote wa Ligi Kuu hadi sasa, wanahitaji pointi tatu leo ambazo zitawafanya waendeleze kile walichokifanya katika mechi nne za ligi zilizopita ambazo wameshinda zote.

Kupoteza mchezo wa leo au kutoka sare, maana yake kutaifanya Simba itengeneze mazingira rahisi kwa watani wao Yanga kuwapa presha kwenye mbio za ubingwa wa ligi msimu huu.

Wageni Azam FC wamepata ushindi katika mechi moja tu kati ya nne walizocheza kwenye Ligi Kuu huku wakitoka sare katika michezo mitatu hivyo ili waendelee kuwa na matumaini ya kutwaa ubingwa wanahitajika kupata ushindi leo.

Kama wakipoteza, maana yake watatanguliwa na Simba kwa pointi tisa na pia kama Yanga ikiifunga Coastal Union, itawapita kwa pointi 10 jambo ambalo ni wazi kwamba litakuwa gumu kwa Azam FC kupita katikati yao wotw na kutwaa ubingwa.

Simba imeonekana kuwa na historia nzuri katika mechi dhidi ya Azam na kuthibitisha hilo, hawajapoteza mechi tano mfululizo za Ligi Kuu dhidi ya timu hiyo inayonolewa na Florent Ibenge ambapo tangu Simba ilipofungwa bao 1-0 na Azam FC, Oktoba 27, 2022, imeshinda mechi mbili zilizofuata na kutoka sare tatu.

Ni mechi ambayo nyota wawili ambao waliitumikia Simba hivi karibuni, Sadio Kanoute na Aishi Manula waliopo ndani ya kikosi cha Azam FC, wanakutana na waajiri wao wa zamani.

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Addis Worku amesema kuwa wanajipanga kuhakikisha wanaifunga Simba leo.

“Kila mechi ni stori, maandalizi na staili tofauti. Mechi na Singida (Black Stars) tulicheza vizuri lakini tulipoteza nafasi nyingi lakini jambo la msingi katika soka ni kutengeneza nafasi na sisi tunafanya hivyo na tunaamini kwamba tutapata ushindi,” alisema Worku.

Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Selemani Matola amesema kwamba timu yake inafahamu ugumu wa mchezo huo na itajitahidi kusaka ushindi.

“Maandalizi yetu yanakwenda vizuri. Tunajua itakuwa mechi ngumu kwa sababu siku zote hakuna mechi rahisi kati ya Simba na Azam. Tunaichukulia mechi hii kwa umuhimu mkubwa na maandalizi yetu yanaenda vizuri. Tutahakikisha kesho (leo) tunapata pointi tatu,” alisema Matola.

Katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, Yanga itakuwa ugenini kukabiliana na Coastal Union kuanzia 1:15 usiku.

Ushindi katika mechi hiyo utaifanya Yanga ifikishe pointi 16 na kusogea hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi na kwa Coastal Union utawapeleka hadi nafasi ya sita wakifikisha pointi 12.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *