Syria. Unamkumbuka Doctor Jawad mwanaume mtanashati aliyesumbua kwenye tamthilia ya Crystal, daktari tajiri aliyempenda binti wa kijakazi (Fay Karam). Upendo huo ukakumbana na vikwazo vingi hasa uoande wa familia yake iliyetamani amuoe binti tajiri Alya Karam ambaye hakuwa anamtaka wala kumpenda.

Katika harakati za kupambania penzi lake kwa binti huyo aliyempenda kwa dhati mambo hayakwenda kama alivyotaka akakumbana na changamoto ya wazazi kukataa uhusiano huo na mwisho wakaachana.

Kwenye tamthilia hiyo iliyotengenezwa nchini Lebanon ilikuwa miongoni mwa kazi zilizopendwa zaidi nchini humo na kuwafungulia milango ya umaarufu zaidi wagizaji hao akiwemo Doctor Jawad.

Sasa Doctor Jawad jina lake halisi ni Mahmoud Nasr ni miongoni mwa waigizaji wakubwa nchini Syria ambao wamejipatia umaarufu mkubwa kupitia ubunifu, kipaji kikubwa na uwezo wa kipekee wa kuigiza.

Amewahi kuigiza katika kazi nyingi za kijamii, kihistoria na mara kadhaa alithibitisha kwamba yeye si msanii wa kawaida, bali ni msanii halisi mwenye uwezo.

ALIPOZALIWA

Mahmoud Nasr alizaliwa katika mji wa Sweida, Syria, Agosti 1983. Alikulia Sweida, akasoma huko hadi alipomaliza elimu ya sekondari kwa ufaulu uliomwezesha kujiunga na masomo ya Uhandisi.

Hata hivyo, alichagua kufuata ndoto yake ya sanaa na alikubaliwa kujiunga na Taasisi ya Juu ya Sanaa za Uigizaji 2002.

Katika mwaka wake wa tatu chuoni alishiriki kwenye tamthilia ‘Nafaq’. Baada ya kusomea uigizaji alihitimu 2006 na kuwa mwanafunzi bora katika darasa lake. Hii ilimpa nafasi ya kupata ufadhili wa masomo kwenda Ufaransa.

Baada ya kurejea Syria, alianza kufundisha katika Taasisi ya Sanaa kama mhadhiri msaidizi, lakini hakudumu muda mrefu kwani aliamua kujikita kikamilifu katika uigizaji.

MWANZO WA SAFARI YAKE

Safari yake ilianza rasmi kwenye televisheni 2007, ingawa alianza kushiriki kwenye kazi akiwa chuoni.

Mwaka 2015 ulikuwa wa mafanikio makubwa kwake kwani alicheza kwenye tamthilia ‘Haraer’ na ‘Waiting for Jasmine’.

Aliigiza kwenye filamu Cherry Letters, ambayo ilipata umaarufu mkubwa na kushinda tuzo mbalimbali Syria na duniani.

Mwaka 2016 aliigiza kwenye filamu ‘Syrians’ na kucheza nafasi kubwa kwenye tamthilia ‘Al-Nadam’, ambayo ilipendwa zaidi katika msimu wa Ramadhani.

MAISHA BINAFSI

Mahmoud Nasr bado hajaoa na hajawahi kufunguka kuhusu mahusiano yake, miongoni mwa vitu anavyopenda ni kutenganisha kabisa maisha yake binafsi na taaluma yake.

Ni msanii anayeepuka vyombo vya habari, mahojiano na kuonekana kwenye vipindi, jambo linalofanya maisha yake binafsi kuwa ya faragha zaidi.

KAULI TATA

Katika moja ya mahojiano machache aliyowahi kufanya, alitoa kauli nzito ambazo zilishtua watu alisema anajutia kuingia katika tasnia ya uigizaji, akidai baadhi ya wakurugenzi alifanya nao kazi hawastahili kuwa nyuma ya kamera.

Aliikosoa pia tasnia ya uzalishaji (production) kwa kuharibu mustakabali wa drama za Syria akitaja hilo linadidimiza ukuaji wa filamu na sio kukuza.

Wasanii wenzake walimshambulia kwa kumkumbusha kuwa aliwahi kutibiwa kuwa aliwahi kuwa na tatizo la afya ya akili na alikiri kwa kusema sio jambo la kushangaza kwani linamkuta yeyote.

“Hakuna cha kuonea haya kuhusu kutafuta matibabu ya matatizo ya kisaikolojia. Ni afya kama nyingine lakini ukweli utabaki kuwa pale pale.”

Kauli hii ilimfanya apongezwe na mashabiki na wadau wa sanaa wakimuona kama mwana mapinduzi kwenye tasnia ya filamu.

Miongoni mwa kazi zake ni Saqf Al-Alam (2006), Ahmed Dayaq Al-Mamar (2007), Khalid bin Al-Walid 2 (2007), Qamar Bani Sham (2008), Zaid bin Haritha, Ask Your Soul (2008), Wajh al-Adala (2008) na Taht al-Qadam (2009).

Nyingine Shita’ Sakhen (2009), Al-Hassan wal-Hussein (2011), Omar (2012) – Zaid bin Al-Khattab, Waiting for Jasmine (2015), Mamalik Al-Nar (2019), Crystal (2023) na Awlad Badiaa (2024).

Mbali na uigizaji, Mahmoud anashiriki katika shughuli za kijamii na mfano ni balozi wa nia njema wa taasisi ya SOS Children’s Villages Syria inayosaidia watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu.

Hii inaonyesha kwamba mbali na kuwa mtu maarufu, lakini anapenda kushirikiana na jamii kwenye mambo muhimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *