Dar es Salaam. Baada ya kuimarika kwa njia za kidijitali za kuuza muziki, mwitikio wa wasanii hasa wale wa Bongofleva kutoa albamu ulirejea lakini kwa mwaka 2025 unaoelekea kuisha, tunaweza kusema wametegeana!.
Hii ni kwa sababu tumeshuhudia idadi ndogo zaidi ya albamu zilizoachiwa na wasanii wakubwa (A-list artist) ukilinganisha na mwaka 2024 na hata miaka ya nyuma kabla ya hapo.
Wengi kwa sasa wanakimbilia kutoa Extended Playlit (EP) ambayo inabeba nyimbo chache na haiwalazimishi kuwa na mpangilio au mtitiriko maalum wa kimaudhui kama ilivyo kwa albamu.
Waliotoa EP mwaka huu ni Jux (A Day To Remember), Mbosso (Room Number 3), Nedy Music (The Voice of The Island), Lava Lava (Time), Yammi (After All), Phina (Melanin Therapy) n.k.
Utakumbuka mwaka uliopita baadhi ya waliotoa albamu ni Roma (Nipeni Maua Yangu), Jay Melody (Therapy), Harmonize (Muziki wa Samia), Young Lunya (Mbuzi) na Stamina (Msanii Bora wa Hip Hop).
Wengine ni Marioo (The God Son), Rayvanny (The Big One) na Zuchu (Peace and Money) ambayo ilikuwa ni albamu yake ya kwanza tangu ametoka kimuziki chini ya WCB Wasafi.
Upande wa EP, kulikuwa na Anjella (The Black Queen), Rayvanny (ZiiBeats Vol.2), Bwana Misosi (Mbona Kimya) na Alikiba (Starter), ikiwa ni EP yake ya kwanza baada ya kutoa albamu tatu.
Je, kwa mwaka 2025 mambo yalikuwa vipi upande wa albamu? Kwa asilimia kubwa mambo yameenda kwa kusuasua sana, ni Darassa, Jay Melody na Lady Jaydee waliofanikiwa kuwapa mashabiki zao albamu mpya.
1. Darassa – Take Away The Pain
Rapa huyu kutokea Classic Music Group (CMG), Februari 7, ndipo aliachia albamu yake, Take Away The Pain (2025) yenye nyimbo 15 zilizotayarishwa na Kaniba Creator, Kapipo Beat, Blvcq Igbo, Foxx Made It, Trone, S2kizzy, Element Eleeeh na Abbah.
Miongoni mwa wasanii walioshirikishwa katika albamu hiyo ni Alikiba, Harmonize, Zuchu, Jay Melody na Mbosso huku wa kimataifa wakiwa ni wawili pekee ambao ni Bien na Jovial, wote wakitokea Kenya.
Darassa aliyetoka kimuziki kupitia wimbo wake, Sikati Tamaa (2012) akimshirikisha Ben Pol, hiyo ilikuwa ni albamu yake pili baada ya hapo awali kuachia, Slave Becomes a King (2020) yenye nyimbo 21.
2. Jay Melody – Addiction
Ni kipaji kilichoibuliwa na Tanzania House of Talent (THT), mnamo Mei 9, ndipo Jay Melody aliachia albamu yake, Addiction (2025) yenye nyimbo 12, huku akiwashirikisha Alikiba, Jux na Mwana FA.
Ikumbukwe Jay Melody aliyetoka na wimbo wake, Goroka (2018), huu ni mwaka wa pili mfululizo anatoa albamu, kitu ambacho mashabiki wake wengi hawakukitarajia.
Albamu yake ya kwanza, Therapy (2024) yenye nyimbo 12, ni miongoni mwa albamu zilizofanya vizuri Bongo mwaka uliopita ikitoa nyimbo maarufu kama Wa Peke Yangu, Siyawezi, 18, Forever na kadhalika.
3. Lady Jaydee – Silver
Silver (2025) ni albamu iliyotoka kwa ajili ya kuadhimisha miaka 25 ya Lady Jaydee katika gemu ya muziki, na iliachiwa Juni 20 ikiwa na nyimbo 25 huku ikishirikisha wasanii kama Fid Q, Rapcha, Frida Amani na Wakazi.
Ni albamu ya kwanza tangu kusaini dili na Universal Music, lebo kubwa ya muziki duniani ambayo imekusudia kumpa fursa ya kupata rasilimali za kiwango cha kidunia katika uzalishaji, usambazaji na masoko.
Na hii ni albamu yake ya 10 baada ya Machozi (2001), Binti (2003), Moto (2005), Shukrani (2007), The Best of Lady Jaydee (2012), Nothing But The Truth (2013), Woman (2017), 20 (2021) na Love Sentence (2023).
WASANII WALIOTEGEA
Kuna mastaa wa Bongofleva waliotangaza kuwa wangeachia albamu mwaka huu ila hadi sasa hawajatekeleza ahadi zao, baadhi yao ni Diamond Platnumz, Nandy na Harmonize.
Diamond ambaye hiyo ingekuwa albamu yake ya nne, alidai albamu hiyo itakuwa ya muziki wa Bongofleva kwa asilimia kubwa na kuwataka mashabiki kukaa mkao wa kula ila hadi sasa haijatoka.
Kwa upande wake Nandy, alisema albamu yake ya pili baada ya The African Princess (2018), ingetoka Novemba lakini ameshindwa kutekeleza ahadi hiyo.
“Albamu itatoka Novemba kwa sababu za msingi kabisa! Tunamalizia baadhi ya kolabo na maandalizi kamili ya albamu yenyewe. Tungependa kutoa burudani katika kipindi tulivu na rahisi kwetu,” Nandy alieleza.
Naye Harmonize alitarajia kutoa albamu yake ya sita mwishoni mwa Novemba lakini baadaye alitangaza kusogeza mbele huku akisisitiza huenda akatoka mwakani.
“Sina uhakika kama albamu yangu itatoka mwaka huu, tunajadili namna ya kuisogeza mbele hadi mwaka ujao ili kuhakikisha kila kitu kimekaa sawa,” alieleza Harmonize kupitia Insta Story.
Ikumbukwe Harmonize amekuwa na utamaduni wa kutoa albamu kila mwaka – mtiririko wake upo hivi; Afro East (2020), High School (2021), Made For Us (2022), Visit Bongo (2023) na Muziki wa Samia (2024).