Madrid, Hispania. Ikiwa usiku ambao Xabi Alonso alihitaji ushindi wa kuokoa nafsi yake pale Bernabeu, ndipo mambo yalipomgeuka. Real Madrid ilianza vizuri, ikatawala mchezo, ikapata bao la mapema kupitia Rodrygo dakika ya 28, lakini makosa ya wachezaji yakaizamisha timu na huenda yakamchimbia kocha wao kaburi.
Madrid iliingia uwanjani ikiwa na presha baada ya mwenendo mbaya katika michezo ya hivi karibuni. Bila Kylian Mbappé ambaye anauguza majeraha bado walikuwa bora kuliko Manchester City, ambao katika dakika za mwanzo walionekana kutopata mwelekeo kabisa.
Mabao mawili ya haraka iliyopata City ndani ya dakika saba yaliipa Madrid huzuni isiyoelezeka. Halaand alifunga bao lake la 51 katika mechi 50 za Ligi ya Mabingwa Ulaya alizocheza.
Kipindi cha pili kilikuwa cha City. Walitawala, wakacheza kwa utulivu, huku Madrid wakionekana kupoteza imani.
Mashabiki wa Madrid walikaa kimya. Wimbo wa klabu ulisikika mwisho wa mchezo, lakini bila sauti za mashabiki, ukawa kama wimbo wa maombolezo.
Madrid hawako vibaya kwenye karatasi kwani wako nafasi ya pili katika msimamo wa LaLiga na wana nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wakiwa katika nafasi ya saba na pointi zao 12 huku wakibakiza mechi mbili ambazo watacheza na Monaco na Benfica.
lakini hali ndani ya klabu ni nzito. Kwani hiki ni kichapo cha pili katika michuano ya Ulaya huku mara zote imepoteza kutoka kwa timu za England.
Ndiyo maana mustakabali wa Alonso unaonekana kuyumba.
Kwa upande wa City, walitimiza malengo yao. Wametoka Bernabéu na ushindi, na sasa katika michezo miwili iliyosalia watacheza na Bodo/Glimt na Galatasaray.
Mambo magumu kwa Alonso
Baada ya filimbi ya mwisho, Alonso alishikana mkono na Pep Guardiola, akainamisha kichwa na kutokomea kwenye njia ya kuelekea vyumba vya kubadilishia nguo.
Huenda ikawa mara ya mwisho kuondoka Bernabeu kama kocha wa Madrid kwani alipewa mechi ya Man City kuhamua hatma yake.