MABOSI wa Yanga wakishirikiana na kocha mkuu wa kikosi hicho, Pedro Goncalves wameanza kupiga hesabu kali ya kuimarisha timu dirisha dogo litakalofunguliwa mapema mwakani.

Katika kuhakikisha eneo la mbele linapata mtu wa maana wa kushirikiana na Prince Dube na Clement Mzize, Yanga imepiga hesabu za kumpiga chini Andy Boyeli na kushusha mashine ya maana kutoka Angola.

Straika mpya anayetajwa kuwa katika akili za mabosi wa Yanga ni Laurindo Dilson Maria Aurelio ‘Dupe’ anayeitumikia pia timu ya taifa ya Angola.

Ipo hivi. Uongozi wa Yanga unaendelea na mazungumzo na klabu ya Sekhukhune United ya Afrika Kusini, ili kusitisha mkataba wa mkopo wa Boyeli kutokana na kushindwa kuendana na kasi ya timu hiyo.

Boyele alijiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu huu kwa mkataba wa mkopo wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kumnunua moja kwa moja mwisho wa msimu 2025/26 endapo atafanya vizuri.

Yanga inamlipa Boyeli 50% ya mshahara, huku sehemu nyingine ya mshahara ikilipwa na Sekhukhune United.

Chanzo cha kuaminika kutoka Yanga kililiambia Mwanaspoti,  uongozi pamoja na Kocha Pedro Goncalves wamefikia makubaliano ya kuachana na straika huyo na kutafuta mshambuliaji mwingine dirisha dogo, huku Depu akitajwa kama ndiye mtu anayepigiwa hesabu.

“Ni kweli kuna mazungumzo yanaendelea baina ya uongozi wa Yanga na ule wa Sekhukhune United, kuhusu kuachana na Boyeli kutokana na kushindwa kuendana na kasi, kwa sasa kinachofanyika sasa ni kutafuta mbadala wake dirisha lijalo,” kilisema chanzo hicho cha kuaminika kutoka ndania Yanga na kuongeza;

“Timu ipo vizuri maeneo mengi linaangushwa na safu ya ushambuliaji hilo uongozi wameliona na kocha pia ametoa mtazamo wake juu ya nini kifanyike ili waweze kuwa na safu bora ambayo itatoa ushindani.”

Chanzo hicho kilisema Boyeli, viongozi pamoja na benchi la ufundi wamefanya mazungumzo kilichobaki ni uongozi wa timu aliyotoka na endapo mambo yakienda vizuri baada ya timu kurudi kutoka mapumziko hatakuwa sehemu ya kikosi.

“Msimu huu Yanga ina washambuliaji watatu Prince Dube, Clement Mzize ambaye ni majeruhi na Boyeli, lakini safu haina makali kama matarajio ya uongozi na hata benchi la ufundi hivyo wameshtuka mapema wanataka kufanya usajili ukizingatia timu ina shiriki michuano mikubwa,” kilisisitiza chanzo hicho na kuongeza;

“Kuna Ligi ya Mabingwa Afrika hatupaswi kutegemea washambuliaji waliopo hawana kasi ya kufumania nyavu za wapinzani anatafutwa mshambuliaji dirisha hili dogo japo sio kazi rahisi kutokana na uchache wa wachezaji kwenye nafasi hiyo ni lazima benki ivunjwe haswa.”

Tangu atue Yanga, Boyeli amefunga mabao mawili tu katika ligi na hana nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza amekuwa akipishana na Dube ambaye ndio panga pangua na imekuwa hivyo baada ya Mzize kuumia.

DEPU ATAJWA

Licha ya mabosi wa Yanga kufanya kwa usiri mtu wa kuchukua nafasi ya Boyeli, lakini taarifa za kispoti zinadokeza straika wa Radomiak Radom ya Poland, ndiye anayetajwa kupigiwa hesabu akibebwa na umri alionao na miaka 25 na uwezo wa kucheka na nyavu.

Straika huyo amewahi kukipiga klabu kadhaa zikiwamo Sagrada Esperanca na Petro Atlelltico.

NAHODHA WA TRA NDANI

Katika hatua nyingine, watetezi hao wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (FA),  inadaiwa imemalizana na nahodha wa TRA United ili atue Jangwani kuimarisha kikosi.

Taarifa zilizolifikia Mwanaspoti ni kwamba, katika kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa, mabosi wa Yanga wamevamia TRA Utd kunasa saini ya nahodha na kiungo Emmanuel Mwanengo ambaye muda wowote kuanzia sasa anaweza kuwa mali ya Jangwani kwani mazungumzo ya pande zote yalikuwa hatua ya mwishoni.

Inadaiwa, Yanga ipo katika hatua za mwisho za kumalizana na Mwanengo anayemaliza mkataba na waajiri wake hao dirisha lijalo ili kumnasa kiulaini.

Yanga ilikuwa katika msako wa muda mrefu kutaka kuinasa saini ya mchezaji huyo, kwani tangu dirisha kubwa walionyesha nia ya kumhitaji lakini mambo yalienda tofauti na mipango yao lakini sasa ni suala la muda mchezaji huyo kuvaa jezi ya kijani na njano.

Taarifa hizo kutoka Yanga zinadai, uongozi wa timu hiyo tayari umemalizana na kiungo huyo kwa kumsainisha mkataba wa miaka mitatu anahesabu siku tu kutua Jangwani.

Mwanaspoti linafahamu Yanga tayari imeshamalizana na Mwanengo, lakini hatua pekee iliyosalia ni kufunguliwa kwa dirisha la usajili na kumtambulisha mchezaji huyo.

“Ni kweli tumekamilisha usajili wa kiungo huyo ambaye tulianza kufanya naye mazungumzo tangu dirisha kubwa, lakini mkataba ulimbana tukashindwana sasa hadi kufikia Januari atakuwa mchezaji wa Yanga kwa makubaliano na kusainishana mkataba,” kilisema chanzo hicho hicho na kuongeza;

“Ni mchezaji  mzuri sina sababu ya kutoa maelezo mengi, mpira ni mchezo wa wazi mdau wa kufuatilia atakuwa anaelewa ninaposema ni kiungo mzuri, wataendelea kuona ubora wake akiwa na jezi za njano na kijani.”

Mwanaspoti lilifanya jitihada za kumtafuta kiungo huyo ili kuzungumzia usajili huo na alikana kumalizana na Yanga, huku akikiri mkataba alionao na TRA unamalizika mwezi ujao na amegomea ofa ya kuendelea kubaki hapo.

“Hakuna mazungumzo yoyote baina yangu na Yanga, tangu waliponitafuta mwanzoni mwa msimu kipindi cha dirisha kubwa hawajarudi kwangu, lakini nina ofa kutoka timu mbalimbali ambazo zinahitaji huduma yangu mambo yakienda vizuri nitakufahamisha.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *