
Sudan Kusini imetuma wanajeshi wake katika nchi jirani ya Sudan kwa lengo kulinda kisima cha kimkakati cha mafuta cha Heglig karibu na mpaka. Haya yamebainishwa jana Alhamisi na Mkuu wa jeshi la nchi siku chache baada ya Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kulidhibiti eneo hilo.
Heglig ni kituo kikuu cha usindikaji wa mafuta ya Sudan Kusini, ambayo yanajumuisha sehemu kubwa ya mapato ya umma ya nchi hiyo. Mafuta mengine yameendelea kusambazwa kupitia Heglig, ingawa kwa viwango vilivyopunguzwa sana.
Vikosi vya serikali ya Sudan na wafanyakazi katika kisima cha mafuta cha Heglig Jumapili iliyopita waliondoka katika eneo hilo ili kuepuka mapigano ambayo yangepelekea kuharibiwa vifaa na zana mbalimbali za kazi.
Jenerali Paul Nang, Mkuu vikosi vya ulinzi vya Sudan Kusini amesema kuwa Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini , Mkuu wa Jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na Mkuu wa wanamgambo wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo wameafiki kutumwa wanajeshi hao huko Heglig.
“Kwa sasa ni wanajeshi wa Sudan Kusini ambao wako huko Heglig,” amesema Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Sudan Kusini, Jenerali Niang.
Mafuta husafirishwa kupitia mfumo wa bomba la Mto Nile hadi katika Bandari ya Sudan katika Bahari Nyekundu kwa ajili ya kuuza nje, na hivyo kulifanya eneo la Heglig kuwa muhimu kwa mapato ya fedha za kigeni za Sudan na kwa Sudan Kusini, ambayo haina bandari na inategemea sana mabomba kupitia Sudan.
Bomba lingine la Petrodar, linaanzia Jimbo la Upper Nile la Sudan Kusini hadi Bandari ya Sudan.
Vita vilivyoanza Aprili 2023 kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF vimevuruga mara kwa mara mtiririko wa mafuta nchini Sudan Kusini, ambayo kabla ya mzozo huo ulikuwa wa wastani wa mapipa 100,000 hadi 150,000 kwa siku kwa mauzo ya nje kupitia Sudan.