Nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) zimeidhinisha rasimu ya “Kanuni ya kuanzisha mfumo wa pamoja wa kuwarejesha raia wa nchi ya tatu wasio na vibali halali vya ukaazi.
Mawaziri wa Mambo ya Ndani wa Umoja wa Ulaya waliokutana huko Brussels, wamepasisha rasimu ya “kanuni ya kuanzisha mfumo wa pamoja wa kuwarejesha makwao raia wa nchi ya tatu wanaoishi bila ya kuwa na vibali halali vya ukaazi. Iwapo rasimu hiyo itaidhinishwa na Bunge la Ulaya, itachukua nafasi ya maagizo ya “Kanuni ya Kurejea” iliyopasishwa mwaka 2008 na kuunda mfumo mmoja wa kuwafukuza wahamiaji katika ngazi ya Umoja wa Ulaya.
Hatua hii imechukuliwa huku Shirika la Amnesty International na makumi ya mashirika na taasisi za kimataifa za kutetea haki za wahamiaji zikionya kuhusu kuidhinishwa rasimu hiyo kwa ajili ya utekelezaji wa mwisho. Badala ya kuzingatia ulinzi, malazi, afya na elimu ya wahamiaji, mpango mpya wa Umoja wa Ulaya unasisitiza udharura wa kuzidishwa kiwango cha kuwafukuza, kuwaweka kizuizini na kuwashikilia wahamiaji katika vituo maalumu wakisubiri kurejeshwa makwao.

Katika miaka ya karibuni na hasa baada ya mgogoro wa Syria, Libya, Afghanistan na pia vita vya Gaza na Ukraine, Umoja wa Ulaya umekabiliwa na wimbi la wahamiaji. Hii ni katika hali ambayo viongozi wa Ulaya wamezidisha sheria za kupata hifadhi na vyeti vya uhamiaji na kuongeza kasi ya kukabiliana na wahamiaji haramu. Sera hii inatakelezwa wakati serikali za nchi za Magharibi zenyewe zikiwa chanzo cha migogoro ya kisiasa, kiuchumi na vita katika maeneo mbalimbali duniani. Kwa maneno mengine ni kuwa, aghlabu ya nchi za Kiafrika na za bara Asia, hususan nchi za Magharibi mwa Asia ambazo hii leo zinashuhudia wimbi kubwa la wahajiri kuelekea Ulaya, zimeathiriwa kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja na sera za kikoloni, kijeshi na kiuchumi za nchi za Ulaya. Kwa mfano, wakimbizi wengi wamelazimika kuzihama nchi na ardhi zao kutokana na sera za uingiliaji kati za Ulaya na nchi nyingine za Magharibi. Pamoja na hayo, Umoja wa Ulaya sasa umeamua kutekeleza sera kali kuhusu uhamiaji badala ya kukubali majukumu yake katika suala hili na kusaidia kutatua migogoro hiyo.
Kuhusiana na suala hili, Jean Marc Zaro mwandishi na mchambuzi anasema: “Umoja wa Ulaya unapasa kulitazama kwa uzito mkubwa suala la uhamiaji na raia wanaotafuta hifadhi, hata hivyo kazi hii haiwezi kufanywa kwa kufunga mipaka na kuzidisha ufukuzaji. Ulaya inapasa kubeba dhima ya vitendo vyake vya kuibuka migogoro duniani ambapo raia wengi wamelazimika kuhama makazi yao.”
Nukta nyingine ambayo ni muhimu katika uwanja huu ni mbinu ya usalama ya Ulaya. Umoja wa Ulaya umeratibu sera zake za yhamiaji kwa msingi wa usalama wa mipaka na kupunguza hatari ya wakimbizi badala ya kujikita katika kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji na kutatua chanzo cha uhamiaji. Kuanzisha vituo vya kuhifadhi wakimbizi katika nchi ya tatu na mchakato wa kuwaweka kizuizini na kuwafukuza katika nchi za Ulaya hupelekea wahamiaji kuzuiliwa katika maeneo nje ya Umoja wa Ulaya ambayo yana usimamizi wa chini wa haki za binadamu. Hatua hii siyo tu kwamba inafanya iwe vigumu zaidi kufuatilia hali za wanaotafuta hifadhi, lakini pia inaweza kuwaweka wale waliorudishwa katika nchi zisizo salama katika hatari ya kuteswa, kunyanyaswa, au ukiukwaji wa haki zao za msingi.

Sera mpya za Umoja wa Ulaya zinazidi kuakisi kusahauliwa majukumu ya kihistoria na kimaadili ya Ulaya, nchi ambazo zenyewe zimehusika katika migogoro mbalimbali duniani. Katika hali ya sasa ambapo vita, migogoro ya kiuchumi na kuhamishwa mamilioni ya watu vinaongezeka siku hadi siku kutokana na uvamizi na uingiliaji kati wa mataifa yenye nguvu duniani, Umoja wa Ulaya, badala ya kusimamisha sera zake za uingiliaji kati, umezidisha sera zisizo za kibinadamu kama vile kubana matumizi na kuzidisha kasi ya kufukuza wahamiaji. Hii ni licha ya madai ya siku zote ya nchi za Ulaya kwamba zinalinda na kutetea maadili na haki za binadamu na zinazishutumu nchi nyingi kuwa zinakiuka haki hizo.
Philip Luther, Mkurugenzi wa Amnesty International Kanda ya Asia Magharibi na Afrika Kaskazini, amesema kuhusu suala hili kwamba: “Mapendekezo mapya (ya nchi za Ulaya) ni hatari kubwa inayotishia haki za binadamu, hasa katika maeneo ya uhuru, usalama wa kibinafsi na upatikanaji wa mchakato wa haki wa kuomba hifadhi.”