Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepasisha rasimu ya azimio linaloitaka Israel kuruhusu kutolewa kwa huduma za kibinadamu pasi na vikwazo na vizingiti katika Ukanda wa Gaza.

Azimio hilo, lililopitishwa jana Ijumaa, aidha linaitaka Israel kuheshimu kanuni za Umoja wa Mataifa na kuzingatia majukumu yake chini ya sheria za kimataifa.

Hatua hii ilianzishwa kujibu maoni ya ushauri ya hivi karibuni kutoka kwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), ikithibitisha tena nafasi ya Israel kama “mamlaka inayokalia kwa mabavu (ardhi za Wapalestina)” na mwanachama wa Umoja wa Mataifa.

Likiungwa mkono na Norway na zaidi ya mataifa mengine 12, azimio hilo lilipasishwa na nchi 139, huku 12 zikipiga kura ya hapana, na 19 zikijizuia kupiga kura.

Kabla ya kura hiyo, Mwakilishi wa Kudumu wa Norway katika Umoja wa Mataifa, Balozi Merete Fjeld Brattested, alionya kwamba, mwaka 2024 ulikuwa miongoni mwa miaka “yenye vurugu zaidi” katika miongo mitatu iliyopita, huku mwaka 2025 ukiendelea kkufuata mwelekeo kama huo.

Haya yanajiri huku Umoja wa Mataifa ukionya kuhusu kuongezeka kwa janga la kibinadamu katika Ukanda wa Gaza kutokana na mvua na baridi kali huko Palestina.

Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ametangaza kuwa, Gaza inakabiliwa na mfumo mpya wa hali ya hewa unaoongeza hatari ya hipothemia (kupungua kwa joto la mwili chini ya nyuzi joto 35 za Celsius) kwa watoto na watoto wachanga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *