
Eritrea ilitangaza jana Ijumaa kwamba imejiondoa katika Jumuiya ya Maendeleo ya Serikali za nchi za Afrika Mashariki, maarufu kama IGAD, huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, akielezea wasiwasi wake kuhusu mvutano kati ya Asmara na Addis Ababa.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Eritrea ilisema katika taarifa yake kwamba Asmara imemfahamisha Katibu Mkuu wa jumuiya ya IGAD kwamba uamuzi wake wa kujiondoa kwenye jumuiya hiyo umekuja baada ya IGAD kupoteza mamlaka yake ya kisheria na kutoweza kurejesha utulivu wa kikanda au kukidhi matarajio ya watu wa Pembe ya Afrika.
Eritrea imeituhumu IGAD kuwa ni chombo cha kisiasa kinachotumika dhidi ya baadhi ya nchi wanachama, ikiashiria Ethiopia, ambayo imekuwa na uhusiano na nchi hiyo jirani.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Eritrea ilianzisha upya uanachama wake mnamo Juni 2023 kwa matumaini ya kuendeleza mchakato wa mageuzi wa jumuiya hiyo, lakini haijaona uboreshaji wowote katika utendaji wake.
Kwa upande wake, IGAD imeelezea masikitiko yake kuhusu uamuzi wa Serikali ya Eritrea wa kujiondoa katika jumuiya hiyo.
Taarifa ya IGAD imesema kwamba uamuzi wa wa Eritrea wa kujiondoa kwenye jumuiya hiyo umechukuliwa bila kuwasilisha mapendekezo halisi au kuingia katika mashauriano kuhusu mageuzi ya kitaasisi au sera maalumu.
Taarifa hiyo imesisitiza kwamba IGAD itaendelea kuwasiliana na serikali ya Eritrea na kuihimiza kufikiria upya uamuzi wake na kujiunga tena kikamilifu na jumuiya hiyo kwa nia njema, katika kuhudumia malengo ya pamoja ya amani, utulivu na maendeleo ya kikanda.
Mnamo 2007, Asmara ilitangaza kujiondoa katika jumuiya hiyo ikipinga tuhuma kwamba Eritrea ilikuwa ikiunga mkono kundi la wanamgambo wa al-Shabaab nchini Somalia. Eritrea ilikanusha tuhuma hizo na kuishutumu Ethiopia kuwa inafanya uchokozi dhidi ya Eritrea na Somalia.
Siku hiyo pia, Asmara aliituhumu IGAD kuwa inaipendelea Addis Ababa.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ijumaa, amezitaka Eritrea na Ethiopia kurejea kwenye makubaliano yaliyomaliza rasmi uhasama kati ya mataifa hayo mawili ya Pembe ya Afrika miaka 25 iliyopita, akionya kuwa mvutano unaoibuka upya unaweza kuhatarisha amani ya eneo hilo.