Watumishi wawili wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, akiwemo Mkuu wa Idara ya Fedha na Afisa Utumishi na Rasilimali Watu, wamesimamishwa kazi kufuatia tuhuma za usimamizi dhaifu wa fedha za miradi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani humo.

Hatua hiyo imeelekezwa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Reuben Kwagilwa, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi OWM–TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Mafia.

Kwagilwa amesema hajaridhishwa na namna fedha za miradi zinavyosimamiwa pamoja na utekelezaji wake, akieleza kuwa tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, Serikali imepeleka zaidi ya shilingi bilioni 24 wilayani Mafia kwa ajili ya miradi ya maendeleo, fedha ambazo zinapaswa kusimamiwa kwa uadilifu na uwajibikaji wa hali ya juu.

Katika hatua nyingine, Kwagilwa amemuagiza Katibu Mkuu OWM–TAMISEMI kutuma timu maalumu kufuatilia mwenendo wa Afisa Utumishi na Rasilimali Watu wa halmashauri hiyo ili kubaini uzingatiaji wa taratibu za kiutumishi.

Aidha, amemtaka Katibu Mkuu kuhakikisha ndani ya siku 21 anapeleka Mkuu wa Idara ya Ujenzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mafia ili miradi ya maendeleo ipate usimamizi wa karibu na kuepusha ucheleweshaji na matumizi yasiyo sahihi ya fedha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *