Madaktari 150 kutoka mikoa saba wamepatiwa mafunzo maalum yenye lengo la kuimarisha utoaji wa huduma kwa wanufaika wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).
Mafunzo hayo kuhusu tathmini za magonjwa yatokanayo na kazi yamefunguliwa jijini Tanga na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Rahma Kisuo na kulenga kuwawezesha madaktari kuongeza uelewa na ujuzi katika kushughulikia masuala ya ajali.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Kisuo amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika mafunzo ya rasilimali watu ili kuhakikisha wafanyakazi wanaopata ajali au magonjwa yatokanayo na kazi wanapata fidia stahiki na kwa wakati tena kwa viwango vya kimataifa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Dkt John Mduma, amesema mafunzo hayo yameandaliwa na WCF ikiwa ni sehemu ya kuuwezesha Mfuko kutekeleza vyema jukumu lake la kutoa huduma za matibabu kwa wanufaika na kufanya tathmini sahihi na kwa wakati pindi mfanyakazi anapoumia au kuugua kutokana na kazi.
Mafunzo hayo yamewakutanisha pamoja madaktari kutoka hospitali za umma na binafsi kuanzia ngazi ya vituo vya afya hadi hospitali za rufaa kutoka mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro; Pwani na Dar es Salaam.
#StarTvUpdate