
Wanajeshi wa Burundi chini ya ulinzi mkali, wamewapokea watu hao waliowasili kupitia mpaka wa Kavimvira. Aidha, kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda limetowa wito kwa askari wote wa Burundi ambao bado wako kwenye ardhi ya Kongo kurejea nchini mwao, likitaja kuwa mamia ya askari wa Burundi wamekamatwa katika mapigano ya hivi majuzi huko Kivu Kusini na kuwa wako salama, na watarejeshwa nchini mwao ikiwa serikali ya Burundi itafanya ombi la kurejea kwao kwa kufuata sheria za kimataifa.
Wakati huohuo, Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binaadamu la Human Rights Watch limetahadharisha kuwa kitendo cha mji wa Uvira kuangukia mikononi mwa waasi wa M23 kunahatarisha usalama wa wananchi eneo hilo la mashariki mwa DRC na kuwataka wadau wote kuwezesha raia wanaokimbia mapigano kuondoka salama na kuhakikisha kuwa misaada ya kibinadamu inawafikia wahitaji wote.