Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Urusi imeiainisha Deutsche Welle (DW), shirika la utangazaji la kimataifa la Ujerumani, kama “shirika lisilotakiwa,” kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Urusi.
Uamuzi huo ulikuwa uliombwa na bunge la Urusi, Duma, tangu mwezi Agosti.
Kwa hatua hiyo, DW inaungana na mashirika mengine kadhaa ya vyombo vya habari, asasi zisizo za kiserikali na taasisi ambazo tayari zimepewa hadhi ya “zisizotakiwa,” yakiwemo Radio Free Europe/Radio Liberty, Bellingcat, CORRECTIV, Reporters Without Borders na TV Rain.
Uainishaji wa “shirika lisilotakiwa” unamaanisha kuwa, chini ya sheria za sasa za Urusi, ushirikiano wowote na shirika hilo unachukuliwa kuwa kosa la jinai na unaweza kuadhibiwa kwa faini kubwa au hata kifungo cha jela.
Hata kushiriki au kusambaza maudhui ya shirika hilo, ikiwemo kupitia mitandao ya kijamii, kunahesabika kuwa kosa la kisheria.
DW imesema nini?
Mkurugenzi Mkuu wa DW, Barbara Massing, amesema hatua ya mamlaka za Urusi ni ishara nyingine kwamba Kremlin inataka kuzima uhuru wowote wa maoni nchini humo.
“Urusi inaweza kututaja kama shirika lisilotakiwa, lakini hilo halitatukatisha tamaa,” alisema katika taarifa yake.
Aliongeza kuwa jaribio hilo jipya la kunyamazisha vyombo huru vya habari linaonyesha wazi dharau ya utawala wa Urusi kwa uhuru wa vyombo vya habari na linafichua hofu yake kwa raia wake wenyewe—wale wanaotafuta taarifa, wanaofikiri kwa kina na wanaotamani kujifunza.
Massing alisema DW itaendelea kusimama imara katika kutoa maudhui ya uandishi wa habari na kuwawezesha watu kuunda maoni yao wenyewe.
Shinikizo linaloongezeka dhidi ya DW nchini Urusi
Katika kipindi cha zaidi ya miaka mitatu iliyopita, DW imezidi kukumbwa na athari za hatua kali za Kremlin dhidi ya mashirika na vyombo vya habari vinavyofadhiliwa kutoka nje ya nchi.
DW imekuwa ikitajwa kama “wakala wa kigeni” nchini Urusi tangu Machi 2022, na kabla ya hapo ilikumbwa na marufuku ya matangazo.
Studio ya DW mjini Moscow ililazimika kuhamishwa, na tovuti yake ilizuiwa kupatikana nchini Urusi katika lugha zote.
Huduma ya DW kwa lugha ya Kirusi ilifikia takribani watumiaji milioni 10 kila wiki mwaka 2025, hasa kupitia maudhui ya video.
Hii inaifanya DW Russia kuwa miongoni mwa huduma 10 zinazotumiwa zaidi ndani ya DW. DW pia hutengeneza kipindi cha kila siku cha dakika 30 cha habari kwa Kirusi, DW Novosti, huku kipindi cha vichekesho Zapovednik kinachotengenezwa mjini Riga kikiendelea kupendwa na watazamaji.
Tangu Machi 2024, vipindi vya DW kwa lugha ya Kirusi pia vimejumuishwa katika kifurushi cha TV-Swoboda (“Uhuru”) kinachosimamiwa na Reporters Without Borders.
Kifurushi hicho kinajumuisha takribani vituo 20 huru vya televisheni na redio kwa lugha ya Kirusi, vinavyorusha matangazo kupitia setilaiti za Eutelsat-Hotbird.
Ili kukwepa udhibiti wa mamlaka za Urusi, DW imeongeza utegemezi wake kwa majukwaa ya kidijitali na kutoa zana za kupita vizuizi, zikiwemo kivinjari cha Tor, huduma za VPN na App ya DW.
“Licha ya udhibiti na kuzuiwa kwa huduma zetu na serikali ya Urusi, huduma ya DW kwa Kirusi sasa inawafikia watu wengi kuliko wakati mwingine wowote,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa DW, Barbara Massing.
Aliongeza kuwa DW itaendelea kuripoti kwa uhuru kuhusu vita vya uvamizi dhidi ya Ukraine na masuala mengine ambayo taarifa zake ni chache nchini Urusi, ili kuwapa watu uwezo wa kuunda maoni yao wenyewe.
DW ni nini?
DW ni shirika la utangazaji wa kimataifa la Ujerumani. Kama chombo huru cha habari, hutoa taarifa na habari zisizoegemea upande wowote katika lugha 32 duniani kote.
DW huzingatia masuala ya uhuru na haki za binadamu, demokrasia na utawala wa sheria, biashara ya kimataifa na haki za kijamii, afya na elimu, pamoja na ulinzi wa mazingira, teknolojia na ubunifu.
Huduma za DW za televisheni, mtandaoni na redio huwafikia watumiaji milioni 337 kila wiki duniani kote.