Afisa mmoja amesema wajumbe wa Marekani wangali wanataka Ukraine kusalimisha udhibiti wa majimbo ya Donetsk na Lugansk kama masharti kwa mazungumzo ya amani na Urusi.
Ukraine inapinga matakwa ya Marekani kwamba iyaondoe majeshi yake kutoka majimbo mawili ya Donbas, ambayo Urusi imeshindwa kudhibiti tangu ilipoivamia Ukraine Februari 2022.
Afisa mmoja kwenye mazungumzo hayo wa upande wa Ukraine ameliambia shirika la Habari la AFP kwamba rais wa Urusi Vladimir Putin anataka kumiliki jimbo hilo. Ameongeza kuwa Marekani inashinikiza Ukraine kuwaondoa wanajeshi wake kutoka majimbo hayo lakini Kiev inapinga.
Afisa huyo amesema inashangaza kwamba Marekani inaegemea upande wa Urusi kwenye suala hilo.
Ujerumani yasema uthabiti wa makubaliano kutegemea hakikisho la usalama kwa Ukraine
Msemaji wa serikali ya UjerumaniStefan Kornelius amesema uthabiti wa makubaliano yoyote ya amani utategemea hakikisho la usalama litakalotolewa kwa Ukraine na kusisitiza kuwa maslahi ya bara zima la Ulaya yako hatarini na yanahitaji kulindwa.
Kulingana na taasisi ya masomo ya vita ya Marekani, Urusiinadhibiti takriban maeneo yote ya jimbo la Lugansk na takriban asilimia 80 ya Donetsk
Uchunguzi uliofanywa siku ya Jumatatu na taasisi ya kimataifa ya kissosholojia ya Ukraine (KIIS), ulionyesha kwamba asilimia 75 ya Waukraine wanapinga kusalimisha jimbo la Donbas.
Kwa siku ya pili Jumatatu, mazungumzo ya Rais Zelensky na wajumbe wa Marekani Steve Witkoff na Jared Kushner, yaliendelea mjini Berlin, yakiangazia pia malengo ya Ukraine kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO, mustakabali wa kiwanda cha nyuklia cha Zaporizhzhia kilichotwaliwa na Urusi na pia masuala kuhusu uchaguzi wa Ukraine.
Hayo ni kulingana na afisa huyo aliyezungumza na AFP na ambaye pia alikanusha ripoti kwamba Ukraine ilikubali kuondoa ombi lake la kujiunga na NATO wakati wa mazungumzo hayo.
Urusi yataka Ukraine ikatae kisheria kujiunga na NATO
Kulingana na Urusi, Ukraine kukataa kujiunga na NATO kisheria ni kipengele muhimu katika mazungumzo ya sasa kuhusu makubaliano ya amani yanayoweza kufikiwa kwa Mzozo huo wa wa Ukraine.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amenukuliwa na vyombo vya Habari vya Urusi akisema suala hilo ni miongoni mwa nguzo kuu na linajadiliwa kwa kina kwa kuzingatia masuala mengine yanayohusiana.
Kuhusu wito wa Rais Trump wa kufanyika uchaguzi, afisa huyo amesema kwamba wanaweza kufanya uchaguzi ikiwa tu watasisitiza, lakini hilo ni suala la kiusalama.
Swali ambalo wanajiuliza ni ikiwa Marekani iko tayari kuishinikiza Urusi kusitisha vita.
Pembezoni mwa mazungumzo hayo, Rais Volodymyr Zelensky amekutana na mwenyeji wake Frank-Walter Steinmeier.
(AFPE/DPAE)