Familia yake imeuambia wakfu wenye jina lake kwamba,  Narges alikamatwa Desemba 12 huku ikidai maafisa wa usalama walimpiga vibaya wakati wa kumkamata.

Narges alikamatwa siku ya Ijumaa (12.12.2025), baada ya kuachiwa mwishoni mwa mwaka jana, kufuatia hatua yake ya kukosoa kifo cha wakili Khosrow Alikordi, kilichotokea katika mazingira ya kutatanisha.

Narges ambaye ni mwanakarakati wa kutetea haki za binaadamu alitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel, akiwa gerezani mwaka 2023, kufuatia miongo mitatu ya kutetea haki za wanawake na kuondolewa kwa adhabu ya kifo nchini Iran.

Kulingana na mwendesha mashitaka mjini Mashhad Hasan Hematifar, Narges pamoja na kakayake Alikordi, walitoa maneno ya kichochezi katika maadhimisho ya kumbukumbu ya mauaji ya wakili huyo, Kaskazini Mashariki mwa mji huo wa Mashhad na kuwataka wafuasi wao kutoa matamshi makali ambayo yanahatarisha amani ya Iran.

Familia ya Narges yasema yuko katika hali mbaya kiafya

Hata hivyo familia ya Narges imeuambia wakfu wa “Narges Foundation” kwamba aliwapigia simu na kuwaambia kuwa kipigo alichopata kilikuwa kikubwa mno na kwamba alipelekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi mara mbili.

Narges Mohammadi, Mwanaharakati wa haki za binaadamu Iran
Narges Mohammadi aliyewahi kushinda Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2023 Picha: Nooshin Jafari/Middle East Images/picture alliance

Familia hiyo imesema hali yake wakati walipokuwa wanazungumza nae haikuwa nzuri.

Narges pia aliiambia familia yake kwamba ametuhumiwa kushirikiana na serikali ya Israel na pia alipokea vitisho vya kifo kutoka kwa maafisa wa usalama.

Mwanaharakati huyo mtetezi wa haki za binaadamu,  aliachiwa huru mwezi Desemba mwaka jana kutoka gereza  la Evin mjini Tehran, baada ya kifungo chake kuahirishwa ili apate nafasi ya kupata matibabu. 

Wakfu wake sasa umetoa wito wa kuachiliwa huru mara moja na bila masharti kwa watu wote waliohudhuria kumbukumbu hiyo, ili kutoa heshima na kuonyesha mshikamano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *