Kupitia mtandao wa kijamii wa X, Mjumbe Maalum wa Rais Donald Trump, Steve Witkoff, aliandika siku ya Jumatatu (Disemba 15) kwamba wawakilishi wa Marekani walikuwa na majadiliano ya kina “juu ya mpango wa vipengele 20 wa amani, ajenda za kiuchumi na masuala mengineyo. Hatua kubwa zimepigwa, na watakutana tena leo asubuhi.”
Ingawa ujumbe huo haukufafanuwa muundo wa mazungumzo ya Jumatatu, lakini kwenye kikao cha Jumapili kilichochukuwa masaa matano, ujumbe huo wa Marekani ulikutana na ujumbe wa Ukraine ukiongozwa na Rais Volodymyr Zelensky.
Jioni ya Jumatatu, Kansela Friedrich Merz wa Ujerumani pamoja na Zelensky walitazamiwa kuhudhuria mazungumzo ya kiuchumi kati ya nchi zao.
Merz alikuwa pia amewaalika viongozi wa mataifa ya Ulaya kwenye chakula cha jioni katika kasri lake baada ya mkutano huo.
Miongoni mwa waliotarajiwa kuhudhuria mazungumzo hayo ni Jenerali Alexus Grynkewich, jenerali wa ngazi za juu wa Marekani kwenye NATO barani Ulaya.
Ukraine yataka Ulaya iibane Marekani
Ukraine, ambayo imekuwa ikikabiliana na uvamizi wa kijeshi wa Urusi tangu mwaka 2022, inasaka uungwaji mkono wa washirika wake kwenye mpango unaopendekezwa na utawala wa Trump kukomesha uvamizi huo.
Akizungumza na waandishi wa habari wa nchi yake, Zelensky alisema hakuwa amepokea jibu lolote kutoka Marekani kuhusiana na mapendekezo yake ya mwisho yaliyotaka mabadiliko kwenye mpango wa amani wa Trump.
Rais huyo wa Ukraine alikiri kwamba mpango huo wa amani unaweza usimpendeze kila mtu, lakini alisisitiza kwamba nchi yake ipo kwenye nafasi madhubuti zaidi kwenye majadiliano.
Alikuwa akirejelea hakikisho la ulinzi kwa nchi yake, kutokana na ukweli kwamba sio pande zote zilizounga mkono pendekezo la Ukraine kujiunga na Muungano wa Kijeshi wa NATO.
Urusi yashikilia msimamo wake
Witkoff alikutana na Rais Vladimir Putin wa Urusi mwanzoni mwa mwezi huu, ambapo Putin aliashiria utayari wake wa majadiliano zaidi lakini hapo hapo akisisitiza kuwa nchi yake ilikuwa na mpango wa kimkakati ambao ingeliendelea kutumia nguvu za kijeshi kama hakukuwa na makubaliano yatakayofikiwa.
Msaidizi maalum wa masuala ya kigeni wa Putin, Yuri Ushakov, alikiambia kituo cha televisheni nchini Urusi hapo jana kwamba nchi yake ina matarajio madodo sana na kile kitakachopatikana kwenye mazungumzo ya Berlin.
“Michango ya Ukraine na serikali za Ulaya kwa mpango wa amani wa Trump haitakuwa ya kujenga sana, na hilo ndilo tatizo.” Alisema mshauri huyo wa mambo ya kigeni wa Putin.
Ushakov aliweka wazi kamwe Urusi isingeliachana na matakwa yake, yakiwemo ya kuitaka Ukraine kujiondowa kikamilifu kwenye majimbo mawili ya mashariki ya Donetsk na Luhansk, ambayo vikosi vyake viliyatwaa lakini bado havijayakalia.