“Sajid Akram, 50, raia wa India, na Naveed Akram, 24, raia wa Australia, waliwasili Ufilipino kwa pamoja mnamo Novemba 1, 2025 kutoka Sydney, Australia,” msemaji wa Ofisi ya Uhamiaji Dana Sandoval alisema.

Wote wawili waliorodhesha jiji la Davao kama kituo chao cha mwisho, alisema. Waliondoka Davao mnamo Novemba 28 na kusafiri hadi Manila kwa ndege ya kuunganisha hadi Sydney, kituo chao cha mwisho, aliongeza.

Mashirika yanayohusiana na wanamgambo wa Islamic State yanaendesha harakati zao mjini Davao kwenye kisiwa cha Mindanao. IS inachukuliwa kuwa Kundi la kigaidi na nchi nyingi.

Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese siku ya Jumanne alisema washambuliaji hao wanaonekana kuathiriwa na itikadi ya Islamic State.

Ripoti za vyombo vya habari vya Australia zilidokeza kwamba wanaume hao wawili walikuwa kwenye kambi ya mazoezi nchini Ufilipino kabla ya shambulio la Jumapili huko Sydney, ambapo watu 15 waliuawa. Akram baba ya Naveed, alipigwa risasi na kuuawa na vikosi vya usalama.

Walikuwa wamepokea “mafunzo kama ya kijeshi” huko, kulingana na ripoti za kituo cha televisheni cha Australia ABC na vyombo vingine, vikinukuu vyanzo vya usalama.

Wawili hao waliwafyatulia risasi watuwaliokuwa wakisherehekea sikukuu ya Kiyahudi ya Hanukkah kwenye Ufukwe huo maarufu duniani wa Sydney.

Polisi ya India imesema kuwa Sajid aliondoka nchini humo miaka 27 iliyopita. Imesema asili yake ni eneo la Hyderabad, na kuwa alihamia Australia kutafuta ajira mnamo Novemba 1998.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *