Akizungumza mjini Geneva Uswisi Türk amesema “Nina wasiwasi mkubwa juu ya kuongezeka kwa mapigano kati ya Jeshi la Sudan, Vikosi vya Msaafa wa Haraka, na Kundi la Harakati za Ukombozi wa Watu wa Sudan-Kaskazini SPLM-N, katika eneo la Kordofan,”
Türk, meihimiza pande zote katika mzozo huo wa Sudan na Mataifa yenye ushawishi kuchukua hatua thabiti mara moja.
Tangu 4 Desemba, raia takriban 104 wamepoteza maisha katika mashambulizi kadhaa ya Ndege zisizo na rubani au droni katika eneo hilo.
Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk (katikati), akihutubia Baraza la Haki za Kibinadamu mjini Geneva.
Raia wanaendelea kupoteza maisha
Katika shambulio moja la kusikitisha lililolenga shule ya chekechea na hospitali katika eneo la Kalogi, Kordofan Kusini, mkuu huyo wa Ofisi ya Haki za Binadamu amesema raia 89 wakiwemo wanawake wanane na watoto 43 waliuawa.
Türk pia amekosoa vikali mauaji ya walinda amani sita wa wa Umoja wa Mataifa katika shambulio la droni kwenye kambi ya Umoja wa mataifa huko Kadugli tarehe 13 Desemba.
Ameonya kuwa “Kuongoza na kufanya shambulio dhidi ya wafanyakazi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kunaweza kuwa ni uhalifu wa kivita”.
Hali ya ghasia iliendelea tarehe 14 Desemba, wakati shambulio la ndege isiyo na rubani kwenye hospitali huko Dilling liliripotiwa kuua angalau watu sita na kujeruhi wengine 12, wakiwemo wafanyakazi wa afya.
Türk amesisitiza kuwa “vituo vya matibabu na wafanyakazi wake vina ulinzi maalumu dhidi ya mashambulizi chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu.”
Historia ya eneo la Kordofan
Eneo la Kordofan limekumbwa na mapigano mara kadhaa katika miaka ya hivi karibuni, likihusisha makabiliano kati ya Jeshi la Sudan, Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF, na makundi ya waasi kama Harakati za Ukombozi wa Watu wa Sudan-Kaskazini SPLM-N.
Raia wanabeba mzigo mkubwa zaidi wa ghasia, huku shule, hospitali, na vituo vya Umoja wa Mataifa vikilengwa katika mashambulizi ya anga na Ndege zisizo na rubani.
Mlipuko huu wa sasa OHCHR inasema unakuja katikati ya mzozo wa kisiasa unaoendelea Sudan kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya 2023 na umeongeza hofu ya janga kubwa la kibinadamu.
Türk amehitimisha taarifa yake kwa wito wa dharura, “Ninawahimiza pande zote katika mzozo na Mataifa yenye ushawishi kuhakikisha mashambulizi yanakoma mara moja na kuzuia ukatili dhidi ya raia.”
Kuongezeka kwa ghasia hivi karibuni kunathibitisha kuzidi kwa janga la kibinadamu nchini Sudan, huku miundombinu ya afya na raia vikilengwa mara kwa mara, na kuongeza hatari kwa maisha ya watu walio hatarini.