
Azimio hilo ni matokeo ya mazungumzo ya kina ya kiserikali yaliyofanyika kabla ya kuwasilishwa na kuzingatiwa katika Mkutano wa Nne wa Ngazi ya Juu wa UNGA kuhusu kinga na udhibiti wa magonjwa yasiyoambukiza pamoja na uendelezaji wa afya ya akili na ustawi, uliofanyika tarehe 25 Septemba 2025.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani la Umoja wa Mataifa WHO, katika hatua inayotajwa kuwa ya kihistoria, azimio hilo lenye kichwa cha habari “Usawa na ujumuishaji: kubadili maisha na riziki kupitia uongozi na hatua dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza na kukuza afya ya akili na ustawi” limekuwa la kwanza kabisa kushughulikia kwa pamoja masuala ya magonjwa yasiyoambukiza na afya ya akili.
Kupitishwa kwake kunafungua ukurasa mpya wa kuharakisha maendeleo ya kimataifa kupitia malengo mahsusi yatakayopimika ifikapo mwaka 2030.
Umuhimu wa azimio hili WHO inasema unaonekana zaidi ikizingatiwa uzito wa changamoto zinazolengwa. Kwa sasa, magonjwa yasiyoambukiza NCDs ndiyo chanzo kikuu cha vifo duniani, yakisababisha vifo vya mapema vya watu milioni 18 kila mwaka, huku zaidi ya watu bilioni moja wakiishi na changamoto za afya ya akili.
Zaidi ya hayo, WHO imesisitiza kwamba magonjwa haya huchochewa kwa kiasi kikubwa na vihatarishi vinavyoweza kuzuilika, ikiwemo lishe isiyo bora, matumizi ya tumbaku na pombe, ukosefu wa mazoezi ya mwili, pamoja na uchafuzi wa hewa. Vihatarishi hivyo vina mchango mkubwa katika kudhoofisha afya ya akili, hali inayozifanya changamoto hizi kuongezeka katika kila nchi na kila jamii.
Hivyo, suala hili linatajwa kuwa dharura si tu ya afya ya umma, bali pia ya tija ya jamii na ukuaji endelevu wa uchumi.
Enzi mpya ya malengo yanayopimika
Kwa kuonesha mabadiliko makubwa ikilinganishwa na ahadi zilizotangulia, azimio jipya linaweka malengo matatu ya kimataifa ya “kuharakisha utekelezaji” yatakayofikiwa ifikapo mwaka 2030.
Malengo hayo ni kupunguza idadi ya watumiaji wa tumbaku kwa watu milioni 150, kuongeza idadi ya watu milioni 150 wanaodhibiti shinikizo la damu, pamoja na kuwezesha watu milioni 150 zaidi kupata huduma za afya ya akili.
Ili kuhakikisha malengo hayo yanatekelezeka, azimio hilo pia linaweka viwango vya wazi kwa mifumo ya kitaifa. Kufikia mwaka 2030, angalau asilimia 80 ya nchi zinatakiwa kuwa na sera, sheria, kanuni na hatua za kifedha zinazohitajika, huku asilimia 80 ya vituo vya huduma za afya ya msingi vikitarajiwa kuwa na dawa muhimu na teknolojia za msingi zinazopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa gharama nafuu.
Pia, takriban asilimia 60 ya nchi zinahimizwa kutekeleza sera za ulinzi wa kifedha zinazopunguza au kufidia gharama za huduma muhimu za magonjwa yasiyoambukiza na afya ya akili.
Aidha, asilimia 80 ya nchi zinatakiwa kuwa na mipango ya kitaifa ya sekta mbalimbali inayotekelezeka, pamoja na mifumo thabiti ya ufuatiliaji na ukusanyaji wa takwimu katika maeneo haya.
Akizungumzia kupitishwa kwa azimio hilo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema “Kupitishwa kwa malengo haya madhubuti ya kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza na kukuza afya ya akili ni ushahidi wa dhamira ya nchi wanachama kulinda afya za wananchi wao. Kwa pamoja, tunaweza kubadili mwelekeo wa magonjwa yasiyoambukiza na afya ya akili, na kuleta afya, ustawi na fursa kwa wote.”
Azimio lenye wigo mpana zaidi kuwahi kutolewa
Mbali na kuweka malengo, azimio hili linaelezwa kuwa pana zaidi kuliko yote yaliyowahi kutolewa awali. Limejumuisha mafunzo yaliyopatikana wakati wa janga la coronavirus“>COVID-19 na kulenga kukabiliana na changamoto mpya zinazoibuka duniani.
Kwa mara ya kwanza, azimio hilo linapanua wigo wa magonjwa yasiyoambukiza kwa kujumuisha maeneo kama afya ya kinywa, afya ya mapafu, saratani za watoto, magonjwa ya ini na figo, pamoja na magonjwa adimu.
Vilevile, linatoa uzito kwa vichocheo vya kimazingira, ikiwemo uchafuzi wa hewa, matumizi ya nishati safi ya kupikia, athari za risasi na kemikali hatarishi.
Sambamba na hayo, azimio linashughulikia hatari zinazoibuka katika enzi ya kidijitali, zikiwemo athari za matumizi ya mitandao ya kijamii, matumizi kupita kiasi ya skrini, maudhui hatarishi, pamoja na changamoto za taarifa potofu na upotoshaji.
Pia, azimio linaweka mkazo wa udhibiti kuhusu sigara za kielektroniki na bidhaa mpya za tumbaku, masoko ya vyakula visivyo na afya yanayolenga watoto, uwekaji wa lebo za mbele kwenye vifungashio vya vyakula, pamoja na jitihada za kuondoa mafuta hatarishi.
Msingi wa ahadi hizi umejengwa juu ya usawa, kwa kuzingatia mahitaji ya watu wanaoishi na magonjwa yasiyoambukiza na changamoto za afya ya akili, jamii zilizo hatarini zaidi kutokana na mabadiliko ya tabianchi, Mataifa Madogo ya Visiwa Vinavyoendelea SIDS, na watu walioko katika mazingira ya dharura za kibinadamu.
Ufadhili na mtazamo wa jamii nzima
Katika kutambua hali ngumu ya kiuchumi inayotishia ufadhili wa sekta ya afya duniani, azimio hili linaweka msisitizo mkubwa zaidi katika suala la rasilimali.
Linazihimiza nchi kuhakikisha upatikanaji wa fedha za kutosha, zinazoaminika na endelevu kupitia kuimarisha mapato ya ndani, kuendeleza ushirikiano wa kimataifa, na kuimarisha mifumo ya pamoja ya ufadhili wa kimataifa.
Zaidi ya hayo, azimio linaweka wazi kuwa magonjwa yasiyoambukiza na afya ya akili “si masuala ya sekta ya afya pekee. Badala yake, yanatajwa kuwa nguzo muhimu za maendeleo endelevu na haki ya kijamii, yakihitaji mbinu ya serikali nzima na jamii nzima”. Hii inajumuisha ushiriki wa asasi za kiraia, washirika wa maendeleo, vijana, watu wenye ulemavu, pamoja na wale wenye uzoefu wa moja kwa moja wa changamoto hizi.
Mwelekeo wa baadaye na uwajibikaji
Kwa ujumla, azimio hili linaimarisha na kujenga juu ya matamko matatu yaliyopita, huku likiweka mwelekeo mpya kuelekea dunia yenye afya bora zaidi, yenye usawa na ustawi.
Linasisitiza umuhimu wa mifumo madhubuti ya uwajibikaji ili kuhakikisha kuwa ahadi zinazotolewa zinaleta matokeo halisi na endelevu.
Kwa mujibu wa azimio hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atawasilisha taarifa ya maendeleo kuelekea malengo ya mwaka 2030 kabla ya kufanyika kwa Mkutano ujao wa Ngazi ya Juu.
WHO, kwa kushirikiana na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa, itaendelea kusaidia nchi wanachama kutafsiri ahadi hizi za kihistoria kuwa hatua za vitendo katika ngazi ya kitaifa, huku ikihakikisha uwajibikaji kuanzia sasa hadi mwaka 2030 na hata baada ya hapo.