Kwa mujibu wa takwimu mpya kutoka ripoti ya Uainishaji Jumuishi wa Hatua za Usalama wa Chakula (IPC), zaidi ya Waafghani milioni 17 wanakabiliwa na uhaba mkali wa chakula msimu huu wa baridi. Hili ni ongezeko la watu milioni tatu ikilinganishwa na Waafghani milioni 14.8 waliokadiriwa kuwa katika hali hiyo mwaka jana (IPC3+).

Utapiamlo

Utapiamlo kwa watoto pia unatarajiwa kuongezeka, ukiwaathiri karibu watoto milioni nne katika mwaka ujao. Huku utapiamlo wa watoto ukiwa tayari umefikia kiwango cha juu zaidi katika miongo kadhaa, na kukiwa na upunguzaji mkubwa usio wa kawaida wa ufadhili kwa mashirika yanayotoa huduma muhimu, upatikanaji wa matibabu unazidi kuwa haba.

Usipotibiwa, utapiamlo kwa watoto ni hatari kwa maisha, na vifo vya watoto vinatarajiwa kuongezeka katika miezi migumu ya baridi wakati chakula kinapokuwa haba zaidi. Viashiria vyote muhimu vinaashiria msimu mkali na mgumu wa baridi unaokuja kwa familia zilizo hatarini zaidi nchini Afghanistan.

“Kwa miezi kadhaa WFP imekuwa ikionya kuhusu dalili wazi za kuongezeka kwa mgogoro wa kibinadamu nchini Afghanistan, na takwimu za hivi karibuni zinathibitisha hofu zetu mbaya zaidi, timu zetu zinaona familia zikikosa mlo kwa siku kadhaa mfululizo na kuchukua hatua kali ili kuendelea kuishi. Vifo vya watoto vinaongezeka, na vina hatari ya kuwa vibaya zaidi katika miezi ijayo.” amesema John Aylieff, Mkurugenzi wa WFP nchini Afghanistan.

media:entermedia_image:3228da45-3971-4589-8b20-bdd9409666e2

© UNICEF/Mark Naftalin

Rasilimali za kibinadamu kusaidia wanawake na watoto wao zinapungua nchini Afghanistan.

Changamoto nyingi wakati mmoja

Afghanistan inajiandaa kwa msimu wa baridi mkali na usio na huruma huku mizozo mingi ikikutana kwa wakati mmoja. Ukame umeathiri nusu ya nchi na kuharibu mazao. Kupotea kwa ajira na uchumi dhaifu kumeathiri mapato na riziki. Matetemeko ya ardhi ya hivi karibuni yameacha familia bila makazi, yakisukuma mahitaji ya kibinadamu kufikia viwango vipya vya juu.

Kurudishwa kwa lazima kutoka Pakistan na Iran kunaongeza zaidi mahitaji, huku Waafghani milioni 2.5 wakirejeshwa Afghanistan tangu mwanzo wa mwaka, wengi wao wakiwasili wakiwa na utapiamlo na bila chochote. Takribani idadi sawa zaidi inatarajiwa kurejea mwaka 2026.

Wakati mgogoro ukiendelea kuongezeka, misaada ya kibinadamu kwa Afghanistan inapungua, na kuwaacha mamilioni bila msaada ambao kihistoria umekuwa ukizuia njaa kali na utapiamlo.

Tunahitaji kurudisha mgogoro wa Afghanistan kwenye vichwa vya habari ili kuwapa waafghani walio hatarini zaidi uangalizi wanaostahili, ni lazima tusimame pamoja na watu wa Afghanistan wanaotegemea msaada muhimu ili kuishi, na kutekeleza suluhu zilizothibitishwa kuelekea urejeshaji wenye matumaini, heshima na ustawi.” ameongeza Aylieff.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *