
Mchezaji wa timu ya taifa ya Ecuador, Mario Pineida, ameuawa kwa kupigwa risasi akiwa na umri wa miaka 33.
Katika taarifa zilizotikisa nchi hiyo, Pineida aliuawa na washambuliaji waliowasili wakiwa kwenye pikipiki kisha kufyatua risasi wakimlenga yeye, mama yake na mwanamke mwingine, kulingana na ripoti za eneo hilo.
Pineida, ambaye aliichezea nchi yake mara tisa kati ya mwaka 2014 na 2021, aliuawa mjini Guayaquil, Jumatano katika eneo la kaskazini mwa jiji hilo.
Mtu mwingine ambaye hakutajwa na polisi pia aliuliwa katika tukio hilo, na wa tatu alijeruhiwa.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ecuador imethibitisha kifo cha Pineida bila kutoa maelezo zaidi.
Klabu ya Barcelona de Guayaquil imesema katika taarifa kwamba mashabiki wao wamesikitishwa na kifo cha Pineida.
Ecuador inatarajiwa kuwa na mwaka wake wenye vurugu zaidi katika rekodi, ikiwa na zaidi ya mauaji 9,000, kulingana na Kituo cha Ufuatiliaji wa Uhalifu Ulioandaliwa cha Ecuador.
Nchi hiyo ilikuwa na vifo 7,063 vya vurugu mwaka jana na rekodi ya vifo 8,248 mwaka 2023.
Rais Daniel Noboa ameapa kupambana na makundi ya kihalifu ambayo yamepanua shughuli zao ndani ya eneo la Ecuador kwa ushirikiano na magenge ya kimataifa ya biashara ya dawa za kulevya.
Mwezi Novemba, mwanasoka mwenye umri wa miaka 16 wa Independiente del Valle alifariki baada ya kupigwa risasi kwa bahati mbaya, naye pia katika jiji la Guayaquil.
Miezi miwili kabla ya hapo, Maicol Valencia na Leandro Yépez, wote wachezaji wa Exapromo Costa, pamoja na Jonathan González wa klabu ya 22 de Junio walifariki kutokana na majeraha ya risasi.
Pineida, ambaye alikuwa beki wa pembeni, alicheza mechi nane na Ecuador lakini hakuwa sehemu ya kikosi kilichofuzu Kombe la Dunia la 2026.
Mchezo wake wa mwisho na Ecuador ulikuwa kwenye Copa América ya 2021, alipoingia kama mchezaji wa akiba dakika za mwisho katika mechi ya hatua ya makundi dhidi ya Brazil. Pia alishiriki kwenye michuano ya mwaka 2017.