Dar es Salaam. Mwili wa Fariala Mbutu, mume wa mwimbaji na kiongozi wa bendi ya Twanga Pepete International, Luiza Mbutu unatarajiwa kuzikwa keshokutwa Jumatatu jijini Dar es Salaam.

Fariala ambaye ni mwanamuziki aliyewahi kutamba na bendi mbalimbali, ikiwamo The Kilimanjaro Connection, Marquiz Original, alikumbwa na mauti juzi jijini wakati akiendelea na matibabu akiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikolazwa kwa wiki moja baada ya kufanyia upasuaji wa tumbo.

Kwa mujibu wa Luiza, mwili wa mumewe utahifadhiwa katika makaburi ya Kwa Kondo yaliyopo Bahari Beach, keshokutwa Jumatatu na kwa sasa msiba upo nyumbani kwa marehemu eneo la Salasala.

Fariala aliyekuwa mtoto wa mwanamuziki nguli wa zamani mwenye asili ya DR Congo (zamani Zaire), Aimala Mbutu aliyewahi kutamba na bendi ya Makassy Orchestra inadaiwa alikuwa akisumbuliwa na tatizo la presha, lakini ghafla aliugua tena tumbo na kuwahishwa Muhimbili.

Kwa mujibu wa Luiza aliyeolewa na Fariala mwaka 2000 na kujaaliwa mtoto mmoja wa kiume aitwae Byran, mwanamuziki huyo aliyekuwa akiipigia The Buffalo inayopiga mahotelini, aliugua ghafla tumbo lililovimba kabla ya kubainika akiwa hospitalini ana tatizo katika mrija wa kupitisha chakula na kufanyia upasuaji wiki moja iliyopita kabla ya mauti kumfika juzi alasiri.

“Alikuwa anasumbuliwa na presha tu, ila akaja kuumwa tumbo ghafla likavimba, tukampeleka Hospitali ya Muhimbili akafanyiwa vipimo akakutwa na tatizo la mrija wa kupitisha chakula umevimba ikabidi wamfanyie upasuaji kwa kupunguza utumbo kisha kuuunga tena baada ya hapo akawa anaendelea na matibabu ndipo mauti yakamfika,” alisema Luiza.

Enzi za uhai wake, Fariala aliyekuwa akicharaza gitaa la besi pamoja na kutunga na kuimba, aliwahi kufanya kazi na Marquiz Original, The Kilimanjaro Connection ya Kanku Kelly sambamba na kutumika katika zingzong za wanamuziki mbalimbali kabla ya kutua The Buffalo.

Wanamuziki na wadau mbalimbali za dansi wametoa salamu za rambirambi na kujitokeza nyumbani kwa marehemu kuomboleza wakisema tasnia hiyo imepata pigo kutokana na mchango wa Fariala enzi za uhai wake na ushirikiano aliokuwa nao mwanamuziki huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *