
Kwa kipindi cha miaka 30, Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) kimejijengea historia ya kipekee kama nguzo muhimu ya ulinzi wa haki, maslahi na utu wa wafanyakazi nchini.
Tangu kuanzishwa kwake, TUICO imekuwa mstari wa mbele katika kusimamia haki za wafanyakazi, kushawishi sera bora za ajira na kujenga mahusiano imara kati ya wafanyakazi, waajiri na Serikali.
TUICO ni chama huru kilichosajiliwa chini na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi Tanzania, kwa lengo la kudai, kulinda na kutetea haki, heshima na maslahi ya wanachama wake na wafanyakazi kwa ujumla. TUICO kiliundwa rasmi mwaka 1995 kufuatia Mkutano Mkuu uliofanyika jijini Arusha. Mpaka kufikia mwaka 2025 chama kimetimiza miaka 30 ya uhai wake.
TUICO kilianzishwa katika mazingira ambayo wafanyakazi walikuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo ukosefu wa ulinzi wa kutosha wa kisheria, mazingira duni ya kazi na sauti dhaifu katika maamuzi yanayohusu ajira. Kuanzishwa kwa TUICO kulilenga kuunganisha sauti za wafanyakazi chini ya mwavuli mmoja wenye nguvu, ili kuhakikisha haki zao zinalindwa na kusikilizwa.
Kwa miaka ya awali, TUICO ilijikita zaidi katika kujenga mifumo ya uendeshaji, kuimarisha uanachama na kutoa elimu ya haki za kazi kwa wafanyakazi katika sekta mbalimbali, ikiwemo viwanda, biashara, huduma na taasisi za fedha.
Katika miaka 30 chama kimepata mafanikio makubwa ambayo kwa muda huu mfupi ni vigumu kuyaorodhesha yote. Hata hivyo kwa kifupi ni kama ifuatavyo:-
Chama kimehamasisha wafanyakazi kujiunga na Chama na sasa kina wanachama 150,000 ambao ni mafanikio makubwa kwani kilipoanza kilikuwa na wanachama 30,000 ambao kiliwarithi kutoka OTTU.
Chama sasa kinahudumia wanachama katika Sekta nne ambazo ni Sekta ya Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha na Huduma na Ushauri wakati kilikuwa na sekta mbili tu yaani Sekta ya Viwanda na Biashara wakati kinaanza.
Chama kina ofisi katika mikoa mikubwa 22, ofisi ndogo tano na ofisi ya Makao Makuu. Ofisi zote zina watumishi wa kutosha wenye weledi na vitendea kazi ikiwemo usafiri wa uhakika hivyo huduma kuwafikia wanachama katika ubora mkubwa na unaokubalika.
Chama kinaongoza kwa kufunga mikataba ya hali bora za kazi. Chama kimefikia uwezo wa kufunga mikataba kati ya 80 – 100 kwa mwaka. Mikataba hii huboresha maslali ya wafanyakazi mahala pa kazi.
TUICO kimekuwa mstari wa mbele kutatua migogoro ya wafanyakazi mahali pa kazi katika ngazi mbalimbali za kutoa haki. Chama kimekuwa kikipokea migogoro takribani 320 kwa mwaka. Kupitia chama wafanyakazi wengi hupata haki na maslahi yao.
Chama kimekuwa kikitoa mafunzo kwa wafanyakazi, wanachama na waajiri juu ya masuala ya vyama vya wafanyakazi. Kwa sasa Chama huendesha semina zaidi ya 10,000 kwa mwaka. Semina hizi huwajengea uwezo washiriki na kupunguza migogoro mahali pa kazi.
Chama kimeendelea kujenga uhusiano mwema na Serikali inayoongozwa na Dk Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kama TUCTA, ATE, ILO, FES, IndustriAll, PSI, DTDA, FNV, BWI, IUF na mashikikisho mengine Duniani. Chama kimepata uzoefu mkubwa katika uendeshaji wa shughuliu za Vyama vya Wafanyakazi.
Chama kinashiriki kikamilifu tangu kuanzishwa kwake katika taasisi za utatu kama vile Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Bodi za Kima cha Chini cha Mshahara (Wage Boards) Baraza la Kazi, Uchumi na Jamii (LESCO), Kamati ya Huduma Muhimu (Essential Services Committee) na bodi mbalimbali katika taasisi za Umma, hivyo kuimarisha utatu wetu.
Safari ya miaka 30 haijakosa changamoto. TUICO imekumbana na mabadiliko ya kiuchumi, mageuzi ya sera, ushindani wa soko huria na wakati mwingine mazingira magumu ya ajira. Hata hivyo, changamoto hizo zimekuwa chachu ya mageuzi, ubunifu na uimara wa shirikisho.
Katika kuadhimisha miaka 30, TUICO inaingia hatua mpya yenye dira ya kuimarisha zaidi ulinzi wa wafanyakazi katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi, hasa katika nyanja za teknolojia, ajira zisizo rasmi na uchumi wa kidijitali.
Dhamira ya TUICO inaendelea kuwa ileile: kutetea haki, utu na ustawi wa wanachama wake na wafanyakazi kwa ujumla nchini, huku ikijenga ushirikiano imara kwa maendeleo endelevu ya taifa.
Safari ya miaka 30 ya TUICO ni ushuhuda wa nguvu ya mshikamano wa wafanyakazi. Ni historia ya mapambano, mafanikio na matumaini mapya. Kadri chama kinavyoendelea kusonga mbele, kinaendelea kubaki kuwa sauti ya wafanyakazi na nguzo muhimu ya haki na maendeleo ya kijamii nchini Tanzania.