MBONI Steven Kibamba amepania kufanya vizuri katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 inayoendelea kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja.

Nyota huyo wa Fufuni FC anayecheza eneo la ushambuliaji, ndiye kinara wa mabao kwenye Ligi Kuu Zanzibar msimu huu 2025-2026 akiwa amepachika mabao 10 katika mechi 15 za duru la kwanza. Pia ana asisti sita zinazomfanya kuhusika kwenye mabao 16 katika mechi 15, huku Fufuni ikiwa kileleni na pointi 30.

Katika kuonyesha moto wake hauzimi, Kibamba ameanza kuuwasha kwenye Kombe la Mapinduzi kwa kufanya mambo mawili makubwa.

Mechi ya kwanza dhidi ya Muembe Makumbi iliyochezwa Desemba 29, 2025, alifunga bao lililoipa pointi moja Fufuni, kisha akachaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo na kulamba kitita cha Sh1 milioni.

Mtihani alionao staa huyo na wenzake ni mechi ijayo dhidi ya Simba ambayo itaamua hatma ya kuendelea ama kuishia makundi katika michuano hiyo.

Timu hizo za Fufuni, Muembe Makumbi na Simba zilizopo kundi B, zinaisaka nafasi moja ya kufuzu nusu fainali ambapo itakayokusanya pointi nyingi ndio itapenya.

Kwa mujibu wa ratiba ya mashindano hayo, Januari 3, 2026, Simba itacheza dhidi ya Muembe Makumbi, kisha Januari 5, 2026 ni dhidi ya Fufuni.

“Jambo la kwanza lilikuwa mechi dhidi ya Muembe Makumbi na tayari limeisha, sasa wanafuata Simba, tunapaswa kujiandaa vizuri kupambana nao kikamilifu.

“Kwanza tutawaheshimu kwa sababu wao ni timu kubwa, lakini kuwaheshimu huko haituzuii kufanya kazi, tunataka kushinda dhidi yao na kusonga hatua inayofuata, katika soka hakuna kinachoshindikana,” amesema Kibamba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *