Benki ya CRDB imemkabidhi Deo Ferdinand Mlawa na wenzake watano zawadi walizojishindia katika droo kubwa ya kampeni hiyo. Mlawa wa Mikocheni Dar es Salaam alitangazwa mshindi wa jumla wa kampeni ya Benki ni Simbanking ya CRDB Desemba 17 na baadae Desemba 30, 2025 akakabidhiwa gari mpya.
Licha ya Mlawa mwingine aliyekabidhiwa zawadi ni Desderius Magombola kutoka Meru mkoani Arusha aliyejishindia gari aina ya Toyota IST New Model. Kutokana na dharura aliyokuwa nayo iliyomzuia kusafiri, zawadi yake ilipokelewa na Isis Nyanda katika hafla fupi iliyofanyika Dar Village jijini Dar es Salaam.
Akikabidhi zawadi hizo, Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na wa Kati wa Benki ya CRDB, Bonaventura Paul amesema magari hayo yote mawili yamekatiwa bima kubwa kutoka CRDB Insurance Compani ambayo ni kampuni tanzu ya Benki ya CRDB pamoja na kujazwa mafuta ‘full tank’ tayari kwa kuingia barabarani.
“Siku zote Benki ya CRDB tunatekeleza ahadi yetu. Leo ni siku ya aina yake kukabidhi Toyota Harrier Anaconda kaka yangu Deo Ferdinand Mlawa kwa bahati hii aliyoipata kutokana na matumizi makubwa ya huduma zetu za Simbanking. Zawadi zetu zilikuwa wazi kwa kila mteja wetu,” amesema Bonaventura.
Kwa mwaka 2025 Benki ya CRDB imetoa zawadi ya magari manne aina ya Toyota IST New Model kwa washindi waliokuwa wanapatikana katika kila robo mwaka. Kwenye droo ya mwisho ambayo ndio kubwa zaidi, gari la tano limetolewa kwa mshindi wa jumla pamoja na wanafunzi wawili wa chuo kikuu kupata ufadhili wa kulipiwa ada na wengine wawili kujishindia simu ya kisasa aina ya iPhone 17 Promax.
Wanafunzi waliopata ufadhili wa kulipiwa ada ni Happiness Chacha anayesoma Chuo cha Usafiri wa Majini (DMI) na John Soka kutoka Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) jijini Dar es Salaam huku Maimartha Seleman wa Keko na Felix Sembwana wa jijini Dar es Salaam wakishinda iPhone 17 Promax.
Kufungwa kwa kampeni hii iliyodumu kwa mwaka mzima, kunafungua milango ya maandalizi ya msimu mpya wa mwaka 2026 hivyo Bonaventura amewaasa wateja wa Benki hiyo kuendelea kutumia huduma za Simbanking kwani katika msimu huu mpya kutakuwa na zawadi nyingi tofauti zitakazotolewa kwa wateja watakaoshinda.