
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani vikali hujuma ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Venezuela na utekaji wa Rais Nicolás Maduro pamoja na mkewe, akieleza kitendo hicho kuwa “mfano dhahiri wa ugaidi wa kiserikali” na ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya wananchi wa Venezuela.
Abbas Araghchi alitoa kauli hiyo Jumamosi jioni katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Venezuela, Yvan Gil Pinto, ambapo walijadili matukio ya hivi karibuni kufuatia hujuma hiyo.
Araghchi amelaani kwa maneno makali utekaji wa rais halali wa Venezuela na mkewe, akisema kitendo hicho ni shambulio la moja kwa moja dhidi ya matakwa ya kitaifa ya Venezuela. Amesisitiza tena msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu wa kuunga mkono wananchi wa Venezuela na serikali yao iliyochaguliwa kidemokrasia.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela ameishukuru Iran kwa msimamo wake wa kimsingi na mshikamano, akibainisha kuwa wananchi na serikali ya Venezuela wameazimia kulinda mamlaka yao ya kitaifa na haki ya kujitawala mbele ya vitisho na sera zisizo halali za Washington.
Mazungumzo hayo yalifanyika katikati ya mvutano unaoongezeka kufuatia matamshi ya Rais wa Marekani, Donald Trump, aliyesema Washington itachukua udhibiti wa Venezuela kwa kipindi cha mpito baada ya utekaji huo. Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari huko Florida, Trump alisema Marekani itaiendesha nchi hiyo hadi pale “mpito salama, sahihi na wa busara” wa madaraka utakapokamilika, na kuongeza kuwa maafisa wa serikali yake watasimamia “uongozi” katika kipindi hicho.