Mbeya. Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, amesema Serikali inaendelea kuthamini mchango wa viongozi na wasomi waliolitumikia taifa kwa uadilifu, weledi na uzalendo.
Itunda ameyasema hayo katika kilele cha Tamasha la Michezo ya Kumbukumbu ya aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), marehemu Profesa Tolly Mbwete akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa.
Tamasha hilo limeandaliwa kwa lengo la kuenzi na kuthamini mchango mkubwa alioutoa Profesa Mbwete katika maendeleo ya elimu ya juu na jamii kwa ujumla.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Itunda amesema kuwa tamasha hilo ni ishara ya mshikamano na umoja wa wananchi, sambamba na kuendeleza kumbukumbu ya watu waliotoa mchango wa kipekee katika maendeleo ya nchi.
Tamasha hilo, ambalo hufanyika kila mwaka, limekuwa jukwaa muhimu la kukutanisha wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Kupitia matukio hayo, wananchi hupata fursa ya kushiriki shughuli za kijamii, michezo na maonesho yanayolenga kuinua hali zao za kiuchumi na kijamii.
Miongoni mwa shughuli zilizovutia wengi ni kilele cha mashindano ya mpira wa miguu yaliyoshirikisha jumla ya timu tisa kutoka kata hizo mbili.
Fainali ya mashindano hayo ilizikutanisha timu za Mapambazuko FC na Itambalila FC kutoka kata za Ulenje na Maendeleo, katika mchezo uliovutia hisia za mashabiki wengi na kuonesha ushindani mkubwa.
Mashindano hayo yalilenga kuibua vipaji vya vijana na kuhamasisha michezo kama chachu ya afya, ajira na mshikamano wa jamii.
Katika mchezo huo timu ya Itambalila FC ilikabidhiwa kombe pamoja na fedha taslimu shilingi milioni moja Sh1 milioni kuwa mshindi wa kwanza, Mapambazuko FC wakiwa washindi wa pili wakipata Sh 500,000, huku mshindi wa tatu akikabidhiwa Sh250,000.
Tamasha hilo pia lilipambwa na maonesho mbalimbali ya kimaendeleo, yakiwemo ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), ambayo ilionesha mbegu bora za mazao yanayostawi katika ukanda huo pamoja na pembejeo za kilimo. Hatua hiyo ililenga kuwajengea wananchi uelewa wa kilimo bora, cha kisasa na chenye tija.
Aidha, Kampuni ya Tigo ilishiriki kwa kuonesha bidhaa na huduma zake, zikiwemo huduma za mawasiliano na kifedha, hatua iliyosaidia kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika shughuli za kila siku.
Itunda alitoa salamu za Beno Malisa, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwa bega kwa bega na wananchi katika kuunga mkono michezo na shughuli zote za maendeleo kwa ustawi wa jamii.
Aidha, Itunda amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anaipa kipaumbele sekta ya michezo nchini.