Klabu ya Manchester United imemfuta kazi kocha wake Ruben Amorim, kutokana na muendelezo wa matokeo yasiyoridhisha akimalizia kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Leeds United jana Jumapili, matokeo yaliyoiacha timu hiyo ikiwa nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka jarida la The Athletic, Darren Fletcher, kocha wa timu ya vijana chini ya miaka 18 wa United na mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, anatarajiwa kuchukua jukumu la ukocha kwa muda.

Mechi ijayo ya United ni dhidi ya Burnley, Jumatano usiku, katika mwendelezo wa Ligi Kuu.

Kauli tata kabla ya kufukuzwa

Akizungumza baada ya sare hiyo ugenini kwenye Uwanja wa Elland Road, Kocha huyo raia wa Ureno, alitoa kauli zilizozua tafrani, akisisitiza kuwa yeye ni meneja wa Manchester United na si kocha, kauli iliyotafsiriwa kama kuukosoa uongozi wa juu wa klabu.

“Itakuwa hivi kwa miezi 18 au mpaka bodi iamue kubadilisha. Sitajiuzulu, nitaendelea kufanya kazi yangu hadi mtu mwingine atakapokuja kunibadilisha,” alisema Amorim.

Kauli hiyo inaaminika kuchochea uamuzi wa haraka wa klabu kumfungashia virago kocha huyo wa zamani wa Sporting CP ya Ureno.

Matokeo mabaya

Katika kipindi chake Old Trafford, Amorim alikumbwa na lawama nyingi kuhusu ukosefu wa kubadilika kimbinu, hasa kutokana na kushikilia mfumo wa 3-4-3.

Ingawa iliripotiwa kuwa United walikuwa wakijaribu mifumo mingine mazoezini, mara nyingi alirejesha mfumo wake aliouzoea.

United ilipata ushindi wa 1-0 dhidi ya Newcastle Desemba 26 wakitumia mfumo wa 4-2-3-1, lakini walirejea 3-4-3 katika mchezo uliofuata dhidi ya Wolves uliomalizika kwa sare ya 1-1.

Kwa jumla, Amorim anaondoka akiwa ameiongoza United kushinda michezo mitatu pekee kati ya 11 ya mwisho, hali iliyozidisha presha kwake.

Gharama kubwa kwa United

Kwa mujibu wa mkataba aliotia saini alipoondoka Sporting, hakuna kipengele cha kuvunja mkataba kwa gharama nafuu.

Hii ina maana Manchester United italazimika kumlipa Amorim mshahara wake wote hadi mkataba wake uliokuwa ukitarajiwa kumalizika mwaka 2027.

United ililipa takribani Euro 11 milioni (Sh32 bilioni) kumsajili Amorim kutoka Sporting, ambako alitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Ureno mara mbili (2021 na 2024) pamoja na Kombe la Ligi la Ureno mara mbili.

Safari isiyoacha alama

Amorim alichukua nafasi ya Erik ten Hag, lakini kwa kipindi cha miezi 14 pekee, hakuonekana kama angeweza kufanya makubwa Old Trafford.

Awali, Amorim alionesha kusita kujiunga na United katikati ya msimu, lakini alishawishiwa kukubali uamuzi ambao sasa umeigharimu kazi yake mapema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *