#HABARI: Watumishi wawili wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida—Afisa Utumishi Bw. Eliah Noah Samata na Mhandisi Bw. Innocent Magadula—wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi na ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo.
Agizo hilo limetolewa leo Januari 05, 2026 na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI (Elimu), Mhe. Reuben Kwagilwa (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Nchi Prof. Riziki Shemdoe (Mb), wakati wa ziara ya kukagua miradi ya elimu na barabara wilayani humo.
Mhe. Kwagilwa amesema Bw. Samata amekuwa kikwazo katika usimamizi wa rasilimali watu, hali iliyochochea uzembe na kuchelewesha huduma. Kwa upande wa Bw. Magadula, ametuhumiwa kusimamia vibaya ujenzi wa shule mpya ya msingi katika eneo la Shule ya Sekondari Grace Mesaki kwa kuruhusu matumizi ya vifaa visivyokidhi viwango na kupunguza vipimo vya ujenzi bila kufuata taratibu, jambo linalohatarisha ubora na usalama wa majengo.