TANZANIA ina malengo makubwa ya kukuza tija katika zao la korosho ikiwa ni pamoja na kubangua korosho zote zinazozalishwa nchini ifikapo mwaka 2030.
Ubanguaji wa korosho nchini ni sehemu muhimu katika sekta ya kilimo inayochangia kuongeza thamani ya zao hilo. Kutokana na umuhimu huo, serikali inawekeza katika ujenzi wa viwanda vya kubangua korosho ili kuongeza thamani ndani ya nchi na kupanua ajira hasa kwa vijana na wanawake.
Aidha, kwa sasa juhudi zimeongezeka kwa serikali kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) kuongeza uzalishaji wa korosho zilizobanguliwa ili kuongeza mapato ya wakulima, kupanua masoko ya nje pamoja na kuleta ushindani katika soko la kimataifa la bidhaa zilizoongezwa thamani.
Baadhi ya wabanguaji wadogo wa korosho (wanawake) kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara wamezungumza na gazeti la HabariLEO kuhusu wanavyonufaika kwa kujipatia mapato na kukuza Uchumi wao kupitia ubanguaji korosho.

Amina Mande ambaye ni mbanguaji mdogo na mfanyakazi katika kiwanda cha kubangua korosho cha Tells One General Supply kilichopo Tandahimba anasema shughuli hiyo inasaidia wanawake wengi na familia zao kujikwamua dhidi ya changamoto za maisha kiuchumi.
“Tunajikimu kimaisha kwa sisi wenyewe akina mama pamoja na kusomesha Watoto; kikubwa tunaiomba serikali iendelee kutuwezesha,” anasema. Amina anafafanua, “Kwa mazingira haya, kwa kweli kila siku tunaposikia kuna kiwanda kinafunguliwa sehemu nyingine tunafarijika sana kwa sababu tunajigawa wengine wanaenda kiwanda hiki wengine kiwanda kingine hivyo, hatujazani katika kiwanda kimoja.”
Anaongeza: “Kadiri viwanda vinavyozidi kutanuka katika maeneo yetu ndivyo na sisi akina mama tunavyopata nafuu ya maisha lakini pia, hii biashara yetu inazidi kutanuka kwa sababu kadiri viwanda vinavyokuwa vingi ubanguaji nao unazidi kukua kwa hiyo ajira zinaongezeka kwetu akinamama na hata vijana wetu nao wanapata fursa ya ajira.”
Mbanguaji mwingine na mfanyakazi katika kiwandani hicho ni Amina Makwangu. Yeye anasema kabla ya kuanza kazi kiwandani hapo, alikuwa akipitia changamoto za kipato kwa sababu licha ya kuwa alikuwa akifanya kazi hiyo, alikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa soko la uhakika la kuuzia korosho zake. Anasema baada ya kufikia katika kiwanda, kipato chake kinaenda vizuri kwa kuwa sasa kuna uhakika wa soko.
“Tangu kuanza kazi katika kiwanda hiki, kwa kweli kipato changu kimezidi kama asilimia 50 hadi asilimia 90 kwa kuwa nina uhakika wa kuuza korosho na nyumbani kwangu mimi na familia yangu maisha yanaenda vizuri tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma,” anasema Amina Makwangu. Anaongeza: “Uwepo wa hivi viwanda ni fursa kubwa sana kwetu.”
Msimamizi wa kiwanda cha Tells One General Supply, Mariamu Chilongo anasema lengo la kuanzishwa kiwanda hicho ni kusaidia wabanguaji wadogo wa korosho hasa wanawake ambao hapo awali walikuwa wakikumbana na changamoto ya masoko.
“Tuliamua kuweka hiki kiwanda kwa ajili ya kuwasaidia akina mama na wabanguaji wadogo wanaoleta mizigo yao hapa, tunazipokea na kuzitunza kwa uangalifu mkubwa sana kwa hiyo tunashukuru kwa hii baraka,” anaeleza. “Ni baraka kwa sababu toka tumefungua hiki kiwanda akina mama wamepata sehemu ya kuuza korosho zao na wengine wengine wamejipatia ajira,” anasema Mariamu.
Mhandisi wa Kilimo wa CBT, Sebastian Kiyoyo anasema Mkoa wa Mtwara una viwanda vya ubanguaji 32 kati ya viwanda 54 vya ubanguaji korosho vilivyopo nchini.

Akiwa mkoani Mtwara hivi karibuni, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka anasema ubanguaji wa korosho nchini unachochea ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya zao hilo na kuzalisha ajira kwa wanawake na vijana.
Anasema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ina kiu kubwa ya kuona ubanguaji wa korosho unaogezeka ili kufikia asilimia 100 ya korosho zote zinazolishwa nchini. Nanauka anasema ujenzi huo wa viwanda utaendelea kunufaisha wanawake na vijana kwa kuzalisha ajira jambo ambalo ndilo dhamira kuu ya serikali.
Kwa mujibu wa Nanauka, dhamira ya serikali katika uzalishaji wa korosho ni kufikia tani milioni 1 ifikapo mwaka 2029/2030. Katika msimu wa mauzo ya koroshoghafi kwa mwaka 2024/2025 uzalishaji ulikuwa zaidi ya tani 500,000 na msimu wa mwaka huu 2025/2026 matarajio ni kuzalisha takribani tani 700,000.
“Kubangua kiwango hiki cha korosho ndani ya nchi kutaongeza thamani kubwa ya zao letu na itasaidia kuongeza chachu ya mnyororo wa thamani na kutengeneza fursa za ajira kwa wanawake na vijana wengi,” anasema. Anasema kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, idadi ya Watanzania inakadiriwa kufikia watu milioni 63 na kati yao, asilimia 70 ambao ni sawa na watu milioni 44 ni vijana na wazee wenye uwezo wa kula korosho.
Aidha, endapo juhudi hizo za kuhamasisha ulaji wa korosho nchini zitaendelea na kufanikiwa kuwashawishi kundi hilo la vijana na wazee kila mmoja kula angalau kilo 5 za korosho, mahitaji ya korosho nchini yataongezeka na kufikia zaidi ya tani 200,000 kwa mwaka zinazotokana na korosho ghafi tani milioni 1.
Nanauka anasisitiza, “Endapo jitihada za kuhamasisha ulaji wa korosho nchini zitafanyika kwa juhudi za kutosha lengo hili tunaamini litafanikiwa kwa kuongeza ubanguaji wa korosho na itaongeza wigo katika soko letu la korosho nchini.”
Mwenyekiti wa Bodi ya CBT, Aloyce Mwanjile anahamasisha Watanzania kula korosho ili pamoja na faida nyingine zikiwamo za kiafya, kuwezesha wakulima wa zao hilo nchini kutokuuza koroshoghafi nje ya nchi. Anasema serikali inaendelea na jitihada mbalimbali kuhakikisha ubanguaji unaofanyika nchini unakuwa wenye tija zaidi kiuchumi.