
Katika taarifa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia imesema “inahifadhi haki ya kuchukua hatua zote zinazofaa za kidiplomasia na kisheria ili kulinda mamlaka yake, umoja wa kitaifa na uadilifu wa eneo lake.”
Somalia imekuwa ikisisitiza kwa miaka mingi kwamba Somaliland ni sehemu isiyotenganishwa ya ardhi yake, na hatua yoyote ya kuitambua inakiuka sheria za kimataifa kuhusu mipaka ya mataifa.
Mkutano maalum wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika uliofanyika jana Jumanne umelaani vikali uamuzi wa Israel wa kuitambua Somaliland na kuhimiza uamuzi huo “ufutwe mara moja.”
Hata hivyo uamuzi wa Israel umeuungwa mkono na Marekani, japo umekosolewa na Misri, Uturuki, Baraza la Ushirikiano la Ghuba lenye nchi sita, pamoja na Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu lenye makao makuu yake Saudi Arabia. Umoja wa Ulaya umesisitiza kuwa mamlaka ya Somalia yanapaswa kuheshimiwa.