Ndani ya Venezuela na nje kumekuwa na maandamano mbali mbali, wengine wakipinga hatua hiyo ya Marekani huku baadhi wakiunga mkono, wachambuzi wanasema wengi wa wanaounga mkono ni raia wa Venezuela wanaoishi nje ya nchi.
Uhispania na nchi tano za Amerika Kusini – Brazil, Chile, Colombia, Mexico, na Uruguay – zimeelezea wasiwasi mkubwa baada ya operesheni hiyo ya Marekani, na kuonya juu ya hatari kwa usalama na utulivu wa kikanda.
Uhispania ndiyo ilikuwa mkoloni wa mataifa hayo.
Rais wa Urusi Vladmir Putin na mwenzake wa China Xi Xinping walishutumu shambulio hilo la Marekani huku wakitangaza utayari wao kushirikiana na watu wa Venezuela.
Trump ni kama sikio la kufa
Afrika Kusini ilipinga waziwazi pia shambulio hilo na kutoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoa kauli ya pamoja ya kulaani uvamizi huo.
Iran ilisema shambulio hilo ni ukiukaji wa haki ya kimataifa na uhuru wa kujitawala.
Ufaransa pia ilisema huo ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.Pia jumuiya ya kimataifa imeshutumu ikiwemo Umoja wa Afrika. EU imeelezea wasiwasi lakini haikushutumu moja kwa moja japo imetoa wito wa kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa.
Trump sasa amekuwa kama sikio la kufa, mbali na uvamizi huo, bado anatishia kuishambulia tena Venezuela iwapo utawala wa muda wa nchi hiyo hautatimiza maagizo yake. Vitisho hivyo vimekwenda mbali zaidi, kwani ametishia pia kuishambulia Mexico, Cuba na Colombia.