Dar es Salaam. Hatimaye mkongwe wa muziki wa dansi na Mwenyekiti wa Bendi ya Twanga Pepeta, Asha Baraka ‘Iron Lady’ ambaye pia kwa sasa ni mbunge wa viti maalumu amejitosa kusaidia afya ya Said Fella ‘Mkubwa Fella.’
Ikiwa zimepita siku chache tangu Sweet Fella, ambaye ni mke wa aliyekuwa meneja wa mwanamuziki Diamond Platnumz na Yamoto Band Mkubwa Fella kuandika kwenye mtandao wake wa Instagram kuhusu mumewe kutengwa na baadhi ya watu wake wa karibu tangu augue. Asha ameiambia Mwananchi kuwa amezungumza na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamaganda John Kabudi.
“Mimi nilichofanya nilijaribu kuwaambia wadau kwa sababu Mkubwa Fella ni mtu ambaye amesaidia kundi kubwa la vijana kupita sanaa na alikuwa diwani kupitia CCM. Kikubwa kinachotakiwa ni kupaza sauti ili waweza kumsaidia nimeongea na watu wake wa karibu bahati nzuri mke wake jana niliongea naye.
“Akanitumia orodha ya vitu ambayo vinahitajika mbali na kurudishwa India kwa mara ya pili. Vitu hivyo ikiwamo vifaa vya kumfanyisha mazoezi, apate wheelchair nzuri ya kisasa ya umeme, ili kuweza kutembea. Nimepata orodha jana usiku mkewe kanitumia na jana ile ile niliongea na Waziri Kabudi uso kwa uso, sio kwa njia ya simu,”amesema.
Asha Baraka amesema Waziri ameomba kutumiwa orodha hiyo ya mahitaji.
“Najua na yeye ataongea na Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa. Hatuwezi kumuacha nitafuatilia kwa karibu na Jumapili tumepanga kwenda kwake kumuona. Mtu akipata matatizo tujaribu kupaza sauti tusisubiri mpaka mtu azidiwe au hata ukiwa na uwezo usisubiri hadi kuishiwa ndio unasema.
“Tujaribu kusema mapema lakini usiposema watu wanakuwa hawajui mfano mimi kwa Mkubwa Fella nilichukua wanamuziki watatu ambao alikuwa anawalea yeye akanipa. Ambao wapo ndani ya Twanga Pepeta ndiyo maana nasema alikuwa analea kundi kubwa la vijana. Sisi Watanzania ni wepesi wa kuchangia lakini hata Serikali inasaidia kutokana na uwezo wake,”amesema Asha.
Hata hivyo, mke wa Fella ameiambia Mwananchi kuwa ni kweli ametuma orodha ya vitu kwa Asha Baraka, hivyo anasubiri taratibu nyingine ziendelee. Huku baadhi ya vitu akivitaja vifaa vya mazoezi vya miguu, mikono na mashine ya presha.
Ikumbukwe Machi ,4, 2025 Mwananchi iliripoti hali ya kiafya ya Mkubwa Fella aliyekuwa akisumbuliwa na presha na kupooza miguu. Hata hivyo Fella alisema afya yake imezidi kuimarika baada ya kutoka India kupata matibabu, ambapo huko India gharama zote aligharamia Diamond Platnumz .
Ilipofika Mei, 2025 Fella alisema kutokana na hali yake kuwa mbaya kwa matatizo hayo. Alikata tamaa ya kupona lakini kwa wakati huo anamshukuru Mwenyezi Mungu kwani anaendelea vizuri.
“Nina furaha kwani kwa sasa naendelea vizuri, hali yangu inaimarika kila siku na nimeanza kufanya mazoezi ya kutembea kila ifikapo jioni.
“Ukweli mimi nimeumwa sana yaani nimeumwa kweli hadi nikawa nimekata tamaa ya kupona, ila namshukuru Mungu sana hadi sasa naweza kuongea na wewe hivi na kutembea vizuri kwa kufanya mzoezi, ilikuwa balaa,” amesema Mkubwa Fella.
Taarifa za kuumwa kwa Said Fella ‘Mkubwa Fella’ ziliibuka kwenye mitandao ya kijamii Januari , 2025 kuwa amepoza miguu huku wengi wakidai Diamond amemtelekeza.
Hata hivyo baada ya kupata taarifa hizo Mwananchi ilimtafuata nyumbani kwake Mbagala kata ya Kilungule, jijini Dar es Salaam na kuzungumza na baadhi ya ndugu zake ambao walidai hali yake haikuwa nzuri hata kuzungumza na mtu kwa muda mrefu alikuwa anashindwa.