
Dar es Salaam. Hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya Venezuela na kumkamata Rais wa nchi hiyo, Nicolas Maduro mwishoni mwa wiki iliyopita imekosolewa na jumuiya za kimataifa.
Asubuhi ya Januari 3, 2026 jeshi maalumu la Marekani lililoendeshwa na agizo la Trump lilifanya operesheni kubwa ya kijeshi nchini Venezuela na kumnyakua Rais Maduro na familia yake huko Caracas na baadaye kumfungulia mashtaka akiwa kizuizini huko Marekani.
Kufuatia hatua hiyo, Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN) wametoa kauli kulaani hatua hiyo huku mataifa mengine yakinyooshea kidole ilichokifanya Marekani kuwa ni tukio linalokiuka sheria za kimataifa na lisilokubalika duniani.
Katika tamko lake dhidi ya Trump, Umoja wa Mataifa (UN) umesema alichokifanya Rais huyo wa Taifa lenye utajiri mkubwa ulimwenguni ni hatua inayohujumu waziwazi, msingi wa sheria ya kimataifa, ukitoa wito kwa jumuiya za kimataifa kuungana kulaani kitendo hicho.
Msemaji wa ofisi ya kusimamia haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, Ravina Shamdasani katika kikao na waandishi wa habari mjini Geneva jana, amesema kitendo cha Taifa moja kuliingilia Taifa jingine kwa namna yoyote ni kinyume na misingi ya sheria za kimataifa.
“Hakuna Taifa ulimwenguni linapaswa kutumia vitisho au nguvu dhidi ya taifa jingine au kuingilia uhuru wa kisiasa wa nchi nyingine,” amesema
Shamdasani ametoa wito kwa jumuiya za Kimataifa kuungana pamoja na kutoa msimamo wa pamoja kuweka wazi kwamba kitendo kilichofanywa na Marekani ni kinyume na sheria ya Kimataifa iliyopitishwa na wanachama wa Umoja wa Mataifa, ambayo Marekani pia iliridhia.
Mbali na UN, Umoja wa Afrika nao umetoa kauli yake kupitia kikao cha baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichoketi kwa dharura kujadili na kukemea kilichofanywa na Marekani nchini Venezuela.
Katika tamko hilo, nchi tatu za Afrika: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Liberia na Somali, ambazo ni wanachama wa baraza hilo wanaoliwakilisha bara la Afrika wamezungumzia wasiwasi wao kuhusu hali hiyo ya kuingiliwa kwa Venezuela na kunyakuliwa kwa Rais Maduro hadi kufikishwa Mahakamani huko Marekani kwa mashitaka mazito.
Akitoa msimamo huo kwa niaba ya Umoja wa Afrika (AU), Balozi wa kudumu wa Liberia katika Umoja wa Mataifa Lewis Garseedah Brown II, amesema Marekani inapaswa kuheshimu sheria ya Kimataifa.
”Nchi tatu za Afrika (A3) zinabaki imara katika ahadi yake kwenye misingi ya sheria ya Kimataifa ikiwemo kushimu kikamilifu uhuru wa mipaka na kila taifa kuwa na uhuru wa kudhibiti mipaka yake, kama ilivyofafanuliwa kwa kina katika mkataba wa Umoja wa Mataifa kwa kuzingatia maslahi ya uthabiti wa kikanda na amani ya Kimataifa” amesema.
Nchi hizo tatu zinazofahamika kama A3 ambazo sio wanachama wa kudumu wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, katika tamko lao la pamoja lenye msimamo wa Umoja wa Afrika pia zimetoa wito wa amani na mchakato endelevu kutafuta suluhisho la mgogoro wa Venezuela na Marekani.
Mbali na tamko hilo, Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi (Ecowas), pia imetoa imeeleza kuwa inafuatilia hali inayoendelea katika Jamhuri ya Venezuela huku ikiwa na wasiwasi juu ya usalama kufuatia hatua zilizochukuliwa na Marekani dhidi ya Taifa hilo huru ikiitaka Marekani kuheshimu uhuru wa mipaka wa mataifa ya wengine.
Mbali na matamko ya asasi hizi za kikanda na kimataifa, Baadhi ya Mataifa makubwa yakiwemo Urusi na China, yameibuka na kulaani hatua ya Marekani kuvamia Taifa huru yakitoa wito kwa Marekani kumuachilia kiongozi wa Venezuela Nicolás Maduro pamoja na mke wake Cilia Flores.
Mabalozi wa mataifa hayo mawili katika Baraza la Umoja wa Mataifa wamekosoa kitendo cha nchi hicho cha Marekani wakikiita ni uchokozi na ukiukaji wa sheria za kimataifa.
Katika kikao maalum cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichofanyika New York, Jumatatu, Urusi na China zimelaani vikali hatua ya Marekani kumkamata kiongozi huyo huku Urusi ikiitaja hatua ya Marekani kama ishara ya kurejea katika enzi ya utawala wa nguvu, machafuko na uhalifu
China kwa upande wake imesema hakuna nchi yoyote inayoweza kujifanya kuwa polisi wa dunia wala kujipa mamlaka ya kuwa hakimu wa kimataifa, huku mataifa mengine kadhaa yakiwamo Cuba, Iran, Colombia na nchi zisizofungamana na upande wowote wakiungana kuinyooshea kidole Marekani.
Mbali na matamko hayo ya mataifa, ndani ya Venezuela kumekuwa na malalamiko huku maandamano ya wananchi yakiripotiwa katika baadhi ya maeneo wakishinikiza kuachiwa huru kwa kiongozi wao huyo tangu alipokamatwa.
Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya siasa na diplomasia ya kimataifa wanaondoa hofu kuwa hawaoni kama hatua hiyo ya Marekani inaweza kuibua mgogoro mkubwa wa kiusalama duniani badala yake wanasema inaweza kuathiri kwa kiasi hali ya utulivu kwa mataifa machache yatakayoguswa moja kwa moja.
“Siyo jambo jema kwa nchi moja kumchukua kiongozi wa nchi nyingine huru na kwenda kumfunga kwao bila kufuata sheria za kimataifa. Sheria za Umoja wa Mataifa zinataka hatua hiyo itolewe kibali na baraza la UN siyo kujichukulia mamlaka, hata hivyo kuhusu amani siioni kama hatua hii itatishia amani ya dunia,” amesema Mwanadiplomasia Denis Konga, katika mahojiano na Mwananchi, leo Jumatano Januari 7, 2026