Mwanza. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, ameielekeza Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuimarisha ukaguzi na usimamizi wa mifumo ya usalama na afya katika maeneo yote ya kazi nchini, hususan katika sekta zenye shughuli hatarishi ikiwemo viwanda na migodi.

Waziri Sangu ametoa maagizo leo Januari 7,2026wakati wa ziara yake ya kikazi katika kiwanda cha kusindika samaki cha Omega Fish Limited kilichopo Jijini Mwanza, ikiwa ni sehemu ya ziara zake za kufuatilia utekelezaji wa sheria za kazi, ajira na mahusiano kazini.

Amesisitiza kuwa ni wajibu wa OSHA kushirikiana kwa karibu na wawekezaji na wamiliki wa maeneo ya kazi ili kuhakikisha mifumo madhubuti ya usalama na afya inasimikwa na kuzingatiwa kikamilifu kwa lengo la kulinda nguvu kazi ya Taifa.

“Serikali ina jukumu la kuhakikisha nguvu kazi inayotumika kutekeleza malengo ya Taifa, ikiwemo Dira ya Taifa ya 2050, inalindwa ipasavyo. OSHA mnapaswa kuwa karibu na wawekezaji ili kuhakikisha usalama na afya vinawekwa mbele,” amesema Waziri Sangu.

Akitolea mfano wa Kanda ya Ziwa, Waziri amesema licha ya OSHA kufanya kazi nzuri katika sekta ya uvuvi, bado kuna changamoto katika sekta nyingine kama sekta ya madini, ambako baadhi ya migodi bubu inaanzishwa bila kufuata taratibu za usalama na afya.

“Ninaiagiza OSHA kufanya ukaguzi wa kina katika maeneo yote ya kazi nchini, yakiwemo ya sekta ya madini, ili kuhakikisha sheria na kanuni za usalama na afya zinafuatwa kwa ukamilifu,” amesisitiza.

Awali, Katibu wa Jumuiya ya Viwanda vya Kusindika Samaki, Onesmo Sule, ameieleza Serikali kuwa changamoto kubwa inayowakabili wasindikaji wa samaki ni upungufu wa malighafi unaotokana na uvuvi haramu, hali inayosababisha viwanda kuzalisha chini ya uwezo wake.

Amesema hali hiyo inaathiri ajira za Watanzania pamoja na kupunguza mapato ya fedha za kigeni.

Changamoto hizo pia zimewasilishwa katika risala ya kiwanda cha Omega Fish Limited iliyosomwa na Ofisa Usimamizi wa Rasilimali Watu wa kiwanda hicho, Zena Marijan, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji.

Akijibu hoja hizo, Waziri Sangu amesema Serikali imezipokea changamoto za wadau wa sekta ya uvuvi na kuahidi kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema ziara ya Waziri imelenga kufuatilia utekelezaji wa sheria na kanuni za usalama na afya mahali pa kazi kwa mujibu wa miongozo ya OSHA.

“Kimsingi tumeridhishwa na namna kiwanda hiki kinavyotekeleza miongozo ya usalama na afya ambayo tumekuwa tukiwapatia,” amesema Mwenda.

Kiwanda cha Omega Fish Limited ni miongoni mwa viwanda 64 vya kusindika samaki nchini, kikijikita katika usindikaji wa samaki aina ya sangara kwa ajili ya masoko ya Ulaya na Asia.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi, sekta ya uvuvi ilichangia asilimia 1.7 ya Pato la Taifa (GDP) mwaka 2023 na kukua kwa asilimia 1.4, huku ikitoa ajira kwa takribani Watanzania milioni 6 katika mnyororo mzima wa thamani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *