
Maandamano makubwa yameenea kote nchini Marekani baada ya wakala wa Idara ya Uhamiaji na Forodha (ICE) kumpiga risasi na kumuua mwanamke huko Minneapolis, huku Makamu wa Rais, JD Vance akitetea hadharani vitendo vya shirika hilo la Shirikisho.
Maandamano makubwa yalifanyika jana Jumatano huko Minneapolis na katika miji mikubwa nchini kote, yakijumuisha maelfu ya waandamanaji waliolaani mauaji hayo na kupinga shughuli za ICE.
Maandamano hayo yalichochewa na mauaji ya Renee Nicole Macklin Good wakati wa operesheni ya Idara ya Uhamiaji na Forodha (ICE) huko Minneapolis, ikiwa sehemu ya msako wa kitaifa dhidi ya wahamiaji ambao umepamba moto zaidi chini ya utawala wa sasa wa Marekani.
Huko Minneapolis, maandamano yameshuhudiwa maeneo kadhaa ya mji huku baadhi ya wakazi waliokuwa na hasira wakishutumu ufyatuaji risasi huo. Waandamanaji walipiga nara “Nenda ukamkamate ICE,” wakidai kwamba maafisa wanaotekeleza sheria ya idara hiyo wanapaswa kumtia nguvuni ajenti wa ICE aliyemuua mwanamke huyo.
Mkusanyiko mkubwa zaidi ulikuwa karibu na eneo la tukio la ufyatuaji risasi, ambalo liko yapata maili moja kutoka mahali ambapo George Floyd aliuawa na afisa wa polisi wa jiji mwaka wa 2020, na kusababisha maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi duniani kote.
Mikusanyiko na maandamano kama hayo yameripotiwa pia katika miji mingine mikubwa ya Marekani, ikiwa ni pamoja na New York, New Orleans, Miami, Seattle na kadhalika.
Huko Los Angeles, wananchi walikusanyika Placita Olvera wakitoa wito wa kukomeshwa uvamizi na kukamatwa wahamiaji, jambo ambalo limeibua hofu kwa jamii za Wamarekani.
Shule za umma za Minneapolis zimefungwa kwa muda “kutokana na wasiwasi wa usalama”.
Macklin Good, aliyekuwa na umri wa miaka 37, alikuwa raia mzaliwa wa Marekani kutoka Colorado ambaye alihamia Minneapolis hivi karibuni na hakuwahi kushtakiwa kwa chochote kinachohusisha utekelezaji wa sheria zaidi ya makosa ya trafiki.