Timu ya wanasayansi wa kimataifa imesema Ijumaa kwamba bahari za dunia zilifyonza kiwango kikubwa cha joto mwaka 2025 na hivyo kuchochea hali ya kuongezeka kwa kina cha bahari, dhoruba kali na matumbawe kufa.
Joto ambalo limekusanyika baharini mwaka jana liliongezeka kwa takriban zettajouli 23 — kiasi sawa na karibu cha miongo minne ya matumizi ya nishati msingi duniani.
Ugunduzi huu — uliochapishwa katika jarida la Advances in Atmospheric Sciences — ulionyesha kiwango cha juu zaidi ya mwaka wowote tangu kulipoanzishwa utunzaji wa kumbukumbu za kisasa mapema miaka ya 1950, watafiti walisema.
Zaidi ya wanasayansi 50 kutoka taasisi 31 za utafiti walitumia vyanzo vingi ikiwa ni pamoja na roboti elfu moja zinazoelea zikifuatilia mabadiliko ya bahari hadi kina cha mita 2,000.
Karina von Schuckmann, mwandishi mwenza wa utafiti huo alisema kuchunguza kina, badala ya mabadiliko ya uso wa bahari, hutoa kiashiria bora zaidi cha jinsi bahari zinavyokabiliana na “shinikizo endelevu” kutokana na uzalishaji wa hewa chafu kutoka kwa binadamu
“Taswira iko wazi: matokeo ya 2025 yanathibitisha kwamba bahari inaendelea kupata joto,” von Schuckmann, mtaalamu wa bahari kutoka taasisi ya utafiti ya Ufaransa Mercator Ocean International, aliiambia AFP.
Bahari ndio mdhibiti mkuu wa joto duniani
Bahari ni mdhibiti mkuu wa hali ya hewa ya Dunia kwa sababu hunyonya asilimia 90 ya joto la ziada katika anga linalosababishwa na usambazwaji wa gesi chafu kama vile kaboni.
Nishati hiyo yote ya ziada ina athari kubwa. Bahari zenye joto huongeza unyevunyevu angani, na kutoa nishati inayochochea vimbunga vya kitropiki na mvua zinazoleta madhara makubwa.
Bahari zenye joto zaidi pia huchangia moja kwa moja katika kuongezeka kwa kina cha bahari — maji huongezeka yanapopata joto — na kufanya hali kuwa ngumu kwenye miamba ya kitropiki, ambayo matumbawe yake huangamia kunapotokea mawimbi ya joto ya baharini kwa muda mrefu.
“Ikiwa Dunia itaendelea kuongeza joto, kiwango cha joto baharini pia kitaendelea kuongezeka, kina cha bahari kitaongezeka na kutakuwepo na rekodi mpya,” alisema von Schuckmann.
Chaguo la binadamu
Ongezeko la joto baharini linatofautiana, kwa kuwa baadhi ya maeneo hupata joto haraka zaidi kuliko mengine. Bahari za kitropiki, Atlantiki Kusini, Mediterania, Bahari ya Hindi kaskazini na Bahari ya Kusini zilikuwa miongoni mwa maji yaliyochukua kiwango cha juu zaidi cha joto kilichorekodiwa mwaka wa 2025.
Mradi tu ongezeko la joto duniani halitashughulikiwa na kiasi cha joto kilichonaswa angani kitaendelea kuongezeka, bahari vina vya bahari vitaendelea kuongezeka kwa viwango visivyovumilika, watafiti walisema.