
Amesema fikra zake mara zote zipo eneo la Mashariki ya kati hasa Iran na Syria, ambako mivutano iliyopo inasababisha mauaji ya watu wengi. Papa Leo ambae ni raia wa Marekani, amesema anayaombea maeneo hayo kuwa na amani kwa manufaa ya jamii kwa ujumla.
Papa anayewaongoza waumini wa kikatoliki bilioni 1.4 duniani, pia amewaombea watu wa Ukraine, kufuatia mashambulizi ya Urusi dhidi ya miundombinu ya taifa hilo jirani.
“Nchini Ukraine, mashambulizi mapya na makubwa zaidi, hasa yanayolenga miundombinu ya nishati, yanawaathiri pakubwa raia, huku hali ya hewa ya baridi ikizidi kuwa mbaya. Ninawaombea wale wanaoteseka na narudia wito wangu wa kukomesha vurugu na kuongezwa kwa juhudi za kufikia amani.”
Juhudi za kuutafutia ufumbuzi mzozo wa Ukraine bado hazijafanikiwa licha ya matumaini ya kupatikana mkataba wa amani yanayotolewa kila wakati na pande hizo hasimu.