Umoja wa Afrika umetangaza hatua hiyo baada ya mkutano wa kilele wa hali ya hewa mjini Addis Ababa, Ethiopia. AU imesema Afrika ina utajiri mkubwa wa madini kuanzia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inayokumbwa na vita hadi Nigeria ambayo ni tajiri wa mafuta lakini umoja huo umesema, mataifa ya Afrika yenye utajiri wa mali asili hayafaidiki na rasilimali zake kutokana na miongo kadhaa ya uporaji wa wakoloni, usimamizi mbaya na ufisadi.

Umoja wa Afrika wenye jumla ya nchi 54 wanachama ulikutana wiki hii kwenye mkutano wa kilele wa hali ya hewa mjini Addis Ababa. Katika taarifa iliyochapishwa baada ya mkutano huo Umoja wa Afrika umesema utafuatilia na kuunga mkono kuanzishwa kwa jumuiya ya nchi zenye utajiri wa madini barani Afrika ili kukuza ushirikiano wa kimkakati na endelevu katika kanda hiyo.

Ethiopia Addis Ababa 2025 | rais wa Angola Joao Lourenco
mwenyekiti wa Umoja wa Afrika rais wa Angola Joao LourencoPicha: Amanuel Sileshi/AFP/Getty Images

Umoja wa wa Afrika umesema hatua hiyo inayoitwa “Mkakati wa Madini Muhimu barani Afrika”, ni njia ya kudhibiti na kutumia utajiri mkubwa wa rasilimali hizo kwa manufaa ya bara Afrika kwa maendeleo yanayozingatia ulinzi wa mazingira.  

Hatua hiyo imefikiwa wakati ambapo Marekani inatazamia kupata madini muhimu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kidemokrasia ya Kongo, kwa lengo la kukabiliana na China inayodhaniwa kuwa inakaribia kuhodhi sekta ya madini yenye faida kubwa nchini Kongo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, alisema mwezi Agosti kwamba Afrika inaweza kuwa bara lenye nguvu kutokana na utajiri wake wa malighafi zinayohitajika zaidi kwa ajili ya teknolojia ya kisasa duniani kote.

Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA) linatarajia kuongezeka mara nne mahitaji ya madini muhimu ifikapo 2040.

Umoja wa Afrika umesema licha ya bara la Afrika kusababisha kwa uchache kabisa uchafuzi wa mazingira duniani, mataifa ya Afrika ndio yanayoathirika zaidi kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na yana uwezo mdogo wa kukidhi gharama za kukabiliana na uchafuzi wa mazingira, ustahimilivu na maendeleo endelevu.

AU imetoa wito wa kutekelezwa ahadi nyingi za kimataifa za fedha na ushirikiano ili kuziba pengo. Lakini wakati huo huo Umoja wa Afrika umesema bara hilo lazima lijitegemee lenyewe, kwa kuimarisha uwezo wao wa kukusanya rasilimali na kufadhili hatua za kulinda mazingira.

Ethiopia | Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Amanuel Sileshi/AFP/Getty Images

Mwaka uliopita kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa wa COP29 nchini Azerbaijan, mataifa tajiri yaliahidi dola bilioni 300 kwa mwaka kwa ajili ya kufadhili juhudi za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa kwenye mataifa yanayoendelea kiwango ambacho nchi za Afrika zimesema hakitoshelezi.

Kwenye mkutano ujao wa COP30 utakaofanyika mwezi Novemba, 2025 Brazil mwenyeji wa mkutano huo imesema moja kati ya malengo yake ni kutafuta njia nyingine za ufadhili ili kuziba pengo la kifedha.

Chanzo:AFP

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *