Serikali ya Tanzania imedhamiria kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya uendeshaji wa viwanda na biashara nchini Tanzania ikiwemo kuboresha mifumo ya utaratibu na usimamizi wa mipango, mikakati na programu za sekta mbalimbali. Lengo kuu ni kufikia malengo ya kiuchumi na kijamii ya maendeleo endelevu kupitia ujenzi wa uchumi wa viwanda wenye ushindani nchini.

Matangazo ya kibiashara

Sekta ya viwanda na biashara ni nguzo muhimu ya uchumi, inayochochea maendeleo endelevu kwa kuongeza thamani ya mali ghafi, kutoa ajira, kuongeza mapato, na kuboresha teknolojia.

Wizara ya Viwanda na Biashara imepata mafanikio makubwa katika sekta ya viwanda na biashara. Mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa kwa mwaka 2024 ulikuwa asilimia 7.3 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2023. Aidha, ukuaji wa sekta ya viwanda ulikuwa asilimia 4.8 mwaka 2024 ikilinganishwa na asilimia 4.3 mwaka 2023.

Sekta ya biashara katika Pato la Taifa kwa mwaka 2024 ulikuwa asilimia 8.6 ikilinganishwa na asilimia 8.4 mwaka 2023. Halikadhalika, kasi ya ukuaji wa sekta ya biashara ilikuwa asilimia 4.8 mwaka 2024 ikilinganishwa na asilimia 4.2 mwaka 2023. Ukuaji huo umechangiwa na uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb) amesema kwa sasa Tanzania  imeendelea kusimamia miradi ya kimkakati ikiwa ni pamoja na Mchuchuma na Liganga, Magadi Soda Engaruka, Makaa ya Mawe Katewaka, Maganga Matitu na Kiwanda cha Kilimanjaro Mashine Tools (KMTC). Katika uendelezaji wa viwanda kwa kutumia malighafi za ndani pamoja na ukuaji wa biashara kwa ujumla.

Katika kipindi cha miaka minne Serikali kupitia wizara ya viwanda na biashara  imefanikiwa katika Mradi Unganishi wa Mchuchuma na Liganga uliopo Ludewa mkoani Njombe nyanda za juu Kusini mwa Tanzania kwa kupata mafanikio  pamoja na ulipaji wa fidia ya Tsh bilioni 15.4 kwa wananchi 1,142 kwa ajili ya Mradi huo.

Mlima Liganga uliopo Ludewa mkoani Njombe Nyanda za juu Kusini mwa Tanzanian ambao unatarajiwa kuchimbwa chuma.
Mlima Liganga uliopo Ludewa mkoani Njombe Nyanda za juu Kusini mwa Tanzanian ambao unatarajiwa kuchimbwa chuma. © Ikulu ya rais

Pia, Serikali kwa sasa iko katika makubaliano ya mwisho ya mradi huo kuanza. Mradi huo unalenga kuendeleza sekta ya viwanda, kuongeza ajira, na kuokoa fedha za kigeni kwa kupunguza uagizaji wa malighafi.

“Wananchi wanapaswa kujiandaa na kuchangamkia fursa hii kwa sababu italeta mabadiliko makubwa ya kiuchumi. Wakinamama waone nafasi ya kupika chakula kwa wafanyakazi, na wakinababa washiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za viwanda hivyo,”

Alisema Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo wakati akizungumzia miaka minne ya serikali ya awamu ya sita.

“Wizara inaendelea kuratibu maandalizi ya mradi wa makaa ya mawe Katewaka, uliopo katika hatua za mwisho za kuanza utekelezaji. Mradi huu, wenye akiba ya tani milioni 100 na uwezo wa kuzalisha tani milioni 1.5 kwa mwaka kwa muda wa miaka 100.  Hadi sasa, Wizara imefanya kikao na mwekezaji na kukamilisha rasimu ya mpango kazi wa utekelezaji“

Alisema waziri Dkt. Selemani Jafo

Kiwanda cha Kilimanjaro Mashine Tools (KMTC)

Wizara kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) ilifanikiwa kufufua Kiwanda cha Kilimanjaro Mashine Tools (KMTC) baada ya kusimama kwa zaidi ya miaka 30. Katika kipindi cha miaka minne (4), Serikali ilitoa takriban Sh4.07 bilioni kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji, na kufikia sasa mashine 47 na vipuri 132 vimezalishwa.

Kiwanda cha kutengeneza Vioo cha Sapphire Float Glass kilichopo Mkuranga Mkoani Pwani. Malighafi zinazotumika kuzalisha vioo zaidi ya asilimia 80 zinapatikana nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na dolomi
Kiwanda cha kutengeneza Vioo cha Sapphire Float Glass kilichopo Mkuranga Mkoani Pwani. Malighafi zinazotumika kuzalisha vioo zaidi ya asilimia 80 zinapatikana nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na dolomite, silca sand, limestone, feldspar pamoja na magadi soda yanayopatikana Engaruka jijini Arusha. © Ikulu ya rais

Kiwanda hicho sasa kinategemewa kwa vipuri na viwanda vya ndani kama TPC, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Kiwanda cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro (KLICL), viwanda vya mkonge, na mashamba ya maua.

Kongani za viwanda vidogo

Kongani za Viwanda Vidogo ni dhana ya mkusanyiko wa viwanda vilivyo katika eneo moja vinavyofanya shughuli zinazotegemeana katika mnyororo wa thamani na kusaidiwa na watoa huduma mbalimbali (Business Development Service Providers – BDSP) katika eneo husika.

Kongani za viwanda vidogo zinatambulika kutokana na umuhimu wake katika kuhamasisha ukuaji wa viwanda na uchumi wa nchi kwa ujumla kwa kuimarisha ushindani, kuongeza tija na ufanisi katika minyororo ya thamani.

Mwaka 2023, Wizara ilifanya utambuzi wa tathmini ya kongani za viwanda vidogo nchini na kubaini uwepo wa kongani za viwanda vidogo zipatazo 40 zilizojikita zaidi katika uongezaji thamani mazao. Aidha, jumla ya maeneo hamsini na tisa (59) yamebainika kuwa na fursa za uendelezwaji wa kongani.

Kongani zilizopo zimeanzishwa kwa jitihada za ofisi za mikoa, halmashauri za wilaya na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (Sido).

Akizungumza Julai 31, 2025, wakati wa ziara ya Dkt, Rais Samia Suluhu Hassan, katika hafla ya uzinduzi wa Kongani ya Viwanda Kwala na Bandari Kavu ya Kwala, Dkt Jafo alieleza kuwa mahitaji ya mwaka ya bidhaa kama mabati yanafikiwa na kuzidi na wazalishaji wa ndani, ikiwa ni ishara ya mafanikio makubwa ya viwanda vya ndani.

“Mahitaji ya mabati kwa mwaka ni tani 130,000, lakini kwa sasa wazalishaji wa ndani kama Lodhia, King Lion na Alaf wamefikia uzalishaji wa tani 260,000. Hii ina maana tuna ziada ya tani 130,000,” alisema Dkt. Jafo, akisisitiza kuwa uzalishaji huo umeondoa hitaji la kuagiza bidhaa hizo nje ya nchi”

Alisema Dkt. Selemani Jafo.

Waziri huyo aliongeza kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara itaendelea kusimamia maono ya Rais Samia ya kuifanya Tanzania kuwa kinara wa uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa kwenda nje ya nchi. Kongani ya Viwanda ya Kwala yenye zaidi ya hekta 1,000, inatarajiwa kuwa na zaidi ya viwanda 200, huku uwekezaji wake ukifikia zaidi ya dola 3 bilioni za Kimarekani, na kutoa mauzo ya zaidi ya Sh6 bilioni kwa mwaka.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Dkt Selemani Jafo akiongea na Wafanyakazi wanaounganisha magari katika Kiwanda cha kuunganisha malori na matipa cha Saturn Corporation Limited kilichopo wilaya ya Kig
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Dkt Selemani Jafo akiongea na Wafanyakazi wanaounganisha magari katika Kiwanda cha kuunganisha malori na matipa cha Saturn Corporation Limited kilichopo wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam © Ikulu ya rais

Changamoto kwenye kongani

Zipo changamoto mbalimbali zinazoikali sekta hii ya kongani za viwanda ikiwemo teknolojia duni inayotumika katika uzalishaji wa bidhaa. Ukosefu wa miundombinu ya majengo, barabara na umeme katika maeneo yaliyotengwa pamoja na uhaba wa malighafi za kutosha.

Serikali imeamua kuanzisha kongani za viwanda vidogo ili kuongeza ushindani wa bidhaa zinazozalishwa nchini na kuziwezesha kulifikia soko la ndani, kikanda na kimataifa. Katika kipindi cha miaka mitano ijayo (2025 – 2030), Serikali inatarajia kuzijengea uwezo kongani 40 zilizopo na kuendeleza kongani 60.

Uanzishaji wa kongani za viwanda vidogo zitasaidia katika kuongeza thamani ya bidhaa zitakazozalishwa na kuziwezesha kushindana katika soko la ndani, kikanda na kimataifa. Hatua hii itaongeza uzalishaji wa ajira nchini kwa kupunguza uuzaji wa mazao ghafi nje ya nchi.

Tanzania ina jumla ya viwanda 13 vya magari, kati ya viwanda hivyo, viwanda viwili vinaunganisha magari ambavyo ni GF-Trucks and Equipment Ltd kilichopo Pwani na Saturn Corporation Limited kilichopo Kigamboni, Dar es Salaam.

Moja ya Kisima cha maji yenye magadi soda katika Mradi wa Kimkakati wa Magadi soda Engaruka uliopo Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha
Moja ya Kisima cha maji yenye magadi soda katika Mradi wa Kimkakati wa Magadi soda Engaruka uliopo Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha © Ikulu ya rais

Viwanda 11 vilivyosalia vinatengeneza matrela. Kiwanda cha GF-Truck kina uwezo wa kuunganisha magari 200 kwa mwezi na kimetoa ajira 300. Kiwanda cha Saturn Corporation kina uwezo wa kuunganisha vichwa vya magari 900 na tipa 270 kwa mwezi na kimetoa ajira za kudumu 250. Kiwanda cha TATA kitakapokamilika kinatarajia kuunganisha vichwa vya magari, tipa pamoja na pikipiki.

Utafutaji wa masoko nje ya nchi

Katika kipindi cha miaka minne, Wizara kupitia TanTrade imeratibu ushiriki wa Tanzania katika matukio mbalimbali ya ukuzaji biashara ndani na nje ya nchi yakiwemo Maonesho ya 45 hadi 48 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, Maonesho ya Bidhaa za Viwanda, Maonyesho ya Expo 2020 Dubai na Maonesho ya Kimataifa ya Mbogamboga na Matunda ya Expo 2020 Doha.

Kupitia matukio hayo, mafanikio mbalimbali yalipatikana yakiwemo ushiriki wa kampuni 20,484 kutoka ndani na nje ya nchi; mauzo ya papo kwa papo yenye thamani ya shilingi bilioni 13.993; na kusainiwa kwa hati za makubaliano 46 baina ya kampuni mbalimbali za ndani na nje ya nchi zenye thamani ya Sh17.52 trilioni katika sekta za usafirishaji, madini, bandari, viwanda, nishati, kilimo, utalii, teknolojia, na tiba. Utekelezaji wa mikataba hiyo imewezesha kuongeza ajira kukuza biashara na uchumi kwa ujumla.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (Mb) na viongozi mbalimbali wakati akiangalia mabomba yanayotengenezwa na kiwanda cha mabomba ya maji na uchakataji pamba cha MOLI Oil Mills Co. Ltd kilichopo Bariadi mkoani Simiyu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (Mb) na viongozi mbalimbali wakati akiangalia mabomba yanayotengenezwa na kiwanda cha mabomba ya maji na uchakataji pamba cha MOLI Oil Mills Co. Ltd kilichopo Bariadi mkoani Simiyu. © Ikulu ya rais

Wizara kupitia WRRB imeendelea kuhamasisha wakulima kutumia mfumo wa stakabadhi za ghala ambapo, katika kipindi cha miaka minne (4) mazao yanayotumia mfumo wa stakabadhi za ghala yaliongezeka kutoka mazao 11 hadi kufikia mazao 16. Mazao hayo ni ufuta, kakao, asali, maharage, mihogo, dengu, choroko, vitunguu swaumu, mahindi, mpunga, mbaazi, korosho, chai, mchele, soya na kahawa.

Kupitia mfumo huo, jumla ya tani 654,928.06 za mazao ziliuzwa na kuwezesha upatikanaji wa Sh4.9 trilioni kwa wakulima na kutengeneza ajira 6,983.

Kwa upande wa miundombinu ya masoko nchini, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Ofisi ya Rais, Tamisemi imeendelea kuboresha mazingira ya kufanyia biashara nchini hususani uboreshaji wa miundombinu kwa ajili ya machinga.

Hadi kufikia Februari, 2025 jumla ya masoko 367 yamejengwa na kuboreshwa katika maeneo mbalimbali nchini. Uwepo wa masoko hayo yamewezesha jumla ya wafanyabiashara ndogondogo 136,041 kuendesha biashara zao katika mazingira rafiki. Kati ya masoko hayo, 16 yamejengwa na kuboreshwa katika mikoa ya Dar es Salaam (Kigogo Fresh, Simu 2000, Mabibo Gamit, Mbezi Luis, Mbezi Njia ya Goba, Buza, Tazara Mbande, na Bunju B), Mbeya (Old Airport), Songwe (Tunduma), Dodoma (Machinga Complex), Arusha, (Engutoto), Mwanza (Mchafukoge), Morogoro (Fire), na Tanga (Kange). Serikali itaendelea kutenga maeneo ya kufanyia biashara na kuyawekea miundombinu rafiki.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Tanzania Mhe Kassim Majaliwa Majaliwa akiwa na Mkewe Bi Mary Majaliwa pamoja na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Saidi Jafo (Mb) wakiwa katika Banda la Tanzania wakati wa Maonesho ya Expo 2025 Osaka Japan.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Tanzania Mhe Kassim Majaliwa Majaliwa akiwa na Mkewe Bi Mary Majaliwa pamoja na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Saidi Jafo (Mb) wakiwa katika Banda la Tanzania wakati wa Maonesho ya Expo 2025 Osaka Japan. © Ikulu ya rais

Hivyo, mafanikio haya yanathibitisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuimarisha uchumi na viwanda, na hivyo kuboresha maisha ya Watanzania. Ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, na wadau wengine ni muhimu ili kufikia malengo haya. Serikali inawahimiza wadau wote, ikiwa ni pamoja na wawekezaji na wananchi, kushirikiana katika kukuza sekta ya viwanda na biashara.

Kudhibiti ubora wa bidhaa, ushindani

Wizara imeendeleza udhibiti wa ubora wa bidhaa kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ambapo leseni 2,569 za nembo ya ubora zimetolewa (1,135 kwa wajasiriamali wadogo), zikiwezesha wazalishaji kufikia masoko ya ndani na nje. TBS pia imesajili bidhaa 6,677 za chakula na vipodozi kutoka nje na kufanya kaguzi za shehena 131,072 kabla ya kuingizwa nchini, bidhaa 286,709 baada ya kuingia, na magari 176,122 yaliyotumika . Leseni hizo zimewezesha wazalishaji kufikia masoko ya ndani na nje ya nchi, hivyo kukuza biashara, kuongeza wigo wa ajira, kupunguza umaskini na hatimaye kukuza uchumi.

Mfanyakazi akiendesha mtambo katika Kiwanda cha kutengeneza vipuri na mitambo mbalimbali cha
Kilimanjaro (KMTC)
Mfanyakazi akiendesha mtambo katika Kiwanda cha kutengeneza vipuri na mitambo mbalimbali cha
Kilimanjaro (KMTC)
© Ikulu ya rais

Wizara kupitia Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) katika kipindi cha miaka minne imefanikiwa kusajili makampuni 58,637, majina ya biashara 109,292, na alama za biashara na huduma 13,153. Vilevile, imetoa Leseni za biashara kundi ‘A’ 65,442, Leseni za Viwanda 1,002 na Hataza 290.

Katika kipindi cha miaka minne (4), Wizara kupitia Wakala wa Vipimo (WMA), imehakiki vipimo 3,410,663. Kati ya vipimo hivyo, vipimo 102,969 vilikutwa na upungufu ambao ulirekebishwa na kuruhusiwa kuendelea kutumika na vipimo 5,607 vilikataliwa. Vipimo vilivyokaguliwa kwa wingi ni pamoja na uhakiki wa pampu za kuuzia mafuta; kiasi cha gesi kwenye mitungi ya gesi; uhakiki wa mizani za kupima nafaka; uhakiki wa malori yabebayo kokoto na mchanga; uhakiki wa usahihi wa ujazo/ kiasi kilichoandikwa cha mbolea na pembejeo kwenye vifungashio husika; uhakiki wa ujazo wa matanki makubwa ya kuhifadhia mafuta na uhakiki wa usahihi wa mizani inayotumika kupima magari ya mizigo na mabasi.

Wafanyakazi wakishona viatu katika Kiwanda cha Kilimanjaro
International Leather Industries kinachojihusisha na uzalishaji wa bidhaa za ngozi. Kiwanda hicho kinamilikiwa na ubia kati ya Jeshi la Magereza na PSSSF na kipo katika Mkoa wa Kilimanjaro
Wafanyakazi wakishona viatu katika Kiwanda cha Kilimanjaro
International Leather Industries kinachojihusisha na uzalishaji wa bidhaa za ngozi. Kiwanda hicho kinamilikiwa na ubia kati ya Jeshi la Magereza na PSSSF na kipo katika Mkoa wa Kilimanjaro
© Ikulu ya rais

Wizara kupitia WMA imefanikiwa kuanzisha vituo vipya vitano katika mikoa yenye mipaka na kufanya kuwa na jumla ya vituo vya ukaguzi 13 Tanzania Bara. Lengo la vituo hivyo ni kuhakiki usahihi wa kiasi/idadi iliyotamkwa (decraled quantity) kwa bidhaa zinazoingia nchini. Vituo hivyo ni Sirari (Mara), Mtukula (Kagera), Namanga (Arusha), Holili (Kilimanjaro), Tunduma (Songwe), Tarakea (Kilimanjaro), Horohoro (Tanga), Kasumulu (Mbeya), Manyovu (Kigoma), Bagamoyo (Pwani), Kwara (Pwani), Bandarini (Dar es Salaam) na Mbweni (Dar es Salaam).

Wizara kupitia WMA imeendelea kufanya uhakiki wa kiasi cha mafuta (jamii ya petroli na mafuta ya kula) yanayoingia nchini kupitia bandari za Dar es salaam, Tanga na Mtwara. Katika kipindi cha miaka minne, jumla ya lita bilioni 30.6 za mafuta kwa meli 546 zilihakikiwa ambazo zimetumika ndani na zile zilizosafirishwa nchi za jirani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *