Trump amesema siku ya Jumapili kwamba ni muhimu sana kulidhibiti eneo hilo la Denmark lenye utajiri wa mafuta kwa ajili ya usalama wa Marekani kwa kuzingatia ongezeko la shughuli za kijeshi za Urusi na China kwenye ukanda wa Arctic.
“Kama hatutaichukua Greenland, Urusi na China wataichukua na sitaruhusu hilo litokee,” Trump aliwaambia waandishi wa habari akiwa kwenye ndege yake ya Air Force One.
Trump amesema yuko tayari kufanya makubaliano na serikali inayojitawala ya kisiwa hicho cha Greenland “lakini kwa namna moja ama nyingine tutaichukua Greenland.”
Denmark na washirika wengine wa Ulaya wameonyesha mshtuko kufuatia vitisho vya Trump kuelekea kisiwa hicho, ambacho kina jukumu la kimkakati kati ya Amerika Kaskazini na Arctic, na ambapo Marekani imekita kambi ya kijeshi tangu Vita vya Pili vya Dunia.
Greenland iliyokuwa koloni la Denmark hadi 1953, iliyoanza kujitawala miaka 26 baadaye na sasa inafikiria kulegeza uhusiano wake na Denmark.
Denmar yasisitiza itaamua yenyewe kuhusu mambo yake
Idadi kubwa ya wakazi wake na vyama vya siasa vimesema havitaki kuwa chini ya udhibiti wa Marekani na vinasisitiza kwamba Wagreenland lazima waamue mustakabali wao wenyewe — mtazamo ambao Trump anaendelea kupingana nao.
“Greenland inapaswa kufanya makubaliano hayo, kwa sababu Greenland haitaki kuona Urusi au China ikiidhibiti,” Trump alionya.
Waziri Mkuu wa Denmark alionya wiki iliyopita kwamba hatua yoyote ya Marekani ya kuichukua Greenland kwa nguvu itaharibu uhusiano wa usalama wa Jumuiya ya Kujihami, NATO uliodumu kwa miaka 80.
Trump alipuuza kauli hiyo akisema: “Ikiwa itaathiri NATO, itaathiri NATO. Lakini unajua, (Greenland) inatuhitaji zaidi kuliko tunavyowahitaji.”
China hata hivyo imeonya siku ya Jumatatu na kuitaka Marekani kutotumia nchi nyingine kama kisingizio cha kufanikisha maslahi yake, kufuatia kitisho hicho cha Trump.
“Arctic inahusu maslahi ya jumla ya jumuiya ya kimataifa,” msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Mao Ning alisema katika mkutano na waandishi wa habari. Alisema shughuli za China katika eneo hilo zinalenga kukuza amani, utulivu, na maendeleo endelevu.